Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuwahimiza wananchi kutoshiriki katika vitendo vya kuwaajiri watoto wala kuruhusu mtu yeyote kujihusisha na vitendo hivyo, huku ikisisitiza kuwa ulinzi wa mtoto ni jukumu la kila mwananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Kazi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Oddo Hekela, wakati akitoa elimu kwa wananchi waliojitokeza katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Hekela amesema kuwa Kifungu cha Tano cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura ya 366, kinakataza ajira kwa mtoto mwenye umri chini ya miaka 14 katika kazi zisizo rasmi kama vile upakuaji wa mizigo, uendeshaji wa magari, pamoja na kazi za viwandani.
"Ni kosa kisheria kumuajiri mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 14, na jamii inapaswa kuelewa kuwa watoto wanahitaji malezi bora yanayowapa nafasi ya kukua kimwili, kielimu, kiafya na kimaadili," alisema Hekela.
Katika banda la Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye maonesho hayo, wananchi wamepata elimu kuhusu madhara ya ajira kwa watoto, ikiwemo athari kwa maendeleo yao, upotevu wa haki za msingi kama elimu, afya, ulinzi dhidi ya unyanyasaji, haki ya kucheza na kupatiwa malezi stahiki.
Ofisi hiyo imeendelea kutumia majukwaa kama Nanenane kutoa elimu ya haki za watoto, huku ikikumbusha jamii kuhusu umuhimu wa kuwalinda watoto dhidi ya kazi hatarishi zinazodumaza ustawi wao wa sasa na baadaye.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED