Mahakama ya Wilaya ya Geita imemhukumu Mganga wa Kienyeji, Nyangeta Mashiku (48), mkazi wa kijiji cha Rudete, Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro, kutumikia kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na nyara za serikali bila kibali halali.
Hukumu hiyo imetolewa leo na Mahakama hiyo baada ya kuridhika na ushahidi uliowasilishwa mahakamani kuthibitisha kuwa mshtakiwa alikuwa na nyara kinyume cha sheria, kitendo kinachokiuka Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori.
Katika tukio la baada ya hukumu, picha iliyoibuka kutoka mahakamani inaonesha mshtakiwa, Nyangeta Mashiku, akiwa amelala chini kwa majonzi huku akilia kwa uchungu baada ya kusomewa adhabu ya kifungo hicho kikali.
Hukumu hiyo inatajwa kuwa onyo kwa watu wote wanaojihusisha na uwindaji haramu na biashara ya nyara za serikali, huku mamlaka zikisisitiza kuwa sheria itachukua mkondo wake kwa yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo hivyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED