KATIKA hali inayozidi kuibua maswali kuhusu afya ya uhusiano wa ndoa, imebainika msongo wa mawazo, maandalizi ya harusi, kutokufahamiana vya kutosha kabla ya kuoana, pamoja na magonjwa ya kimya kimya, ni miongoni mwa sababu zinazochangia vifo vya wanandoa wapya.
Wataalamu na wadau wa masuala ya ndoa wanatoa tahadhari kwa maharusi kuhakikisha wanachukua tahadhari za kiafya na kiakili kabla ya kuingia katika maisha ya ndoa, ili kuepuka maumivu yanayoweza kuzuilika.
Mwenyekiti wa Chama cha Washehereshaji Tanzania (SAA), Stephen Mwakajumba, anasema baadhi ya vifo hutokea wakati au baada ya harusi, kutokana na mashinikizo ya maandalizi na migogoro ya uhusiano.
“Vifo vinavyotokana na msongo wa maandalizi ni vya kweli. Wapo waliopata shambulio la moyo, presha au hata kisukari kutokana na mkazo wa harusi,” anasema.
“Wengine hufumaniwa katikati ya maandalizi na kuona maisha yamevunjika.” Mwakajumba anataja pia kutopima afya kabla ya ndoa kuwa sababu kuu ya vifo vya ghafla, ambapo baadhi ya maharusi huingia katika ndoa wakiwa na maradhi kama ya moyo au shinikizo la damu bila kujua.
Aidha, anagusia changamoto za kifamilia zinazotokea pale ambapo familia haikubaliani na chaguo la kijana wao. Anaeleza pia kuwa hali ya sasa imebadilika ambapo baadhi ya vijana hufikia uamuzi wa kuoana bila kuelewana vya kutosha au kufuata taratibu za kimila.
“Wengine huvalishana pete ya uchumba kabla hata ya kutoa mahari. Hapo ndipo hutokea migogoro na mshtuko mkubwa pale mmoja anapogundua mwenzake ana uhusiano mwingine,” anaeleza.
Katika tukio moja lililotajwa, bibi harusi alifariki dunia baada ya kugundua mchumba wake ana mwanamke mwingine na tayari ana mtoto naye.
Kwa upande wake, Mzalishaji wa vipindi katika Wasafi Media, Onesmo Abraham, anahusisha baadhi ya vifo hivi na masuala ya kiroho na mfumo wa maisha ya kisasa.
“Baadhi ya wanandoa maisha yao yalikuwa na mafanikio kabla ya ndoa, lakini matatizo huanza punde tu baada ya kuoana. Ni muhimu kuingia katika ndoa kwa kumtanguliza Mungu na kufuata maadili ya kiimani,” anashauri.
Abraham pia anatoa angalizo kuhusu zawadi wanazopokea maharusi, akisisitiza kuwa baadhi zinaweza kubeba laana endapo hazijaombewa.
Aidha, anatahadharisha dhidi ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu na tabia ya kuacha wapenzi wa muda mrefu kwa njia zisizofaa.
“Ukimwacha mtu, achana naye kwa amani. Usimwumize kihisia, kwani maumivu hayo yanaweza kuathiri maisha yake kwa kiasi kikubwa,” anasisitiza.
Katika kipindi cha wiki mbili pekee, mshehereshaji maarufu Joshua Mwakabela ameposti matukio mawili ya vifo vilivyohusiana na harusi.
Tukio moja likihusisha bibi harusi aliyefariki dunia kabla ya harusi, na lingine likimhusisha bwana harusi aliyefariki dunia siku chache baada ya harusi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED