Meneja wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Andrew Kisaka, amesema vyombo vya habari vikishindwa kutumika kwa weledi katika kipindi cha uchaguzi vinaweza kuchochea machafuko makubwa, kama ilivyotokea katika baadhi ya nchi za Afrika.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, Kisaka alitoa mifano ya matukio ya machafuko yaliyotokea nchini Nigeria na Kenya kutokana na matumizi mabaya ya vyombo vya habari.
"Nchini Nigeria, baada ya uchaguzi, watu zaidi ya 800 walipoteza maisha. Vilevile nchini Kenya zaidi ya watu 1,000 waliuawa na wengine takribani 600,000 kupoteza makazi yao. Hii yote ilitokana na uchochezi uliosambazwa kupitia vyombo vya habari," amesema Kisaka.
Amesisitiza kuwa waandishi wa habari na vyombo vyao wana jukumu kubwa la kuhakikisha taarifa zinazotolewa ni sahihi, za haki na zisizo na lengo la kuchochea vurugu au migogoro.
“Ni muhimu kuzuia kusambaza taarifa za uongo, kutoa majukwaa kwa watu wenye lugha ya uchochezi, na kujenga taswira potofu dhidi ya vyama vya siasa – hasa vya upinzani,” ameongeza.
Kisaka pia amewakumbusha waandishi kuwa wanayo dhamana ya kuelimisha jamii kuwa wanasiasa wa vyama mbalimbali ni Watanzania wenye haki sawa na mawazo tofauti ya kisiasa, na si maadui wa umma.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED