Tabasamu la faraja, nyakati hizi ni dawa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:20 PM Aug 04 2025
Tabasamu
Picha: Mtandao
Tabasamu

NYAKATI ziwapo ngumu, ni kweli ngumu kwa mtu, ni maisha binadamu, humpata mtu watu Japo huwa hazidumu, kuzibeza sithubutu, tabasamu la faraja, nyakati hizi ni dawa

Upo wakati majira, kilichopo mbele kiza, hata uwe na hasira, mambo yanakuumiza
Mambo yendi bila dira, na usijekuteleza, tabasamu la faraja, nyakati hizi ni dawa

Siku vitu haviendi, kila ugusacho sicho, si kwamba haupendi, yanakutoka tu macho
Waweza kiri ushindi, hata ukiwa maficho, tabasamu la faraja, nyakati hizi ni dawa

Zipo nyakati ni mbaya, hata zuri usione, yalivyo maisha haya, hatari ni usinene
Fungua mapema taya, nafuu ufungamane, tabasamu la faraja, nyakati hizi ni dawa

Muda ni tiba nafuu, ngoja mambo yawe sawa, ondoa mambo makuu, na uepuke ukiwa
Na njia iliyo kuu, ni nguvu kutoishiwa, tabasamu la faraja, nyakati hizi ni dawa

Mshairi: Dk. Raymond Mgeni 

Dk. Raymond Nusura Mgeni, ni daktari wa afya na magonjwa ya akili. Kwa sasa anasomea masomo ya ubingwa eneo hilo katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Shirikishi Muhimbili (MUHAS)

raymondpoet@gmail.com 
+255 676 559 211