Dk. Mollel adai mkewe, msaidizi wake kutekwa, awatuhumu wapinzani wake

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 03:41 PM Aug 04 2025
Dk. Godwin Mollel.
Picha: Mtandao
Dk. Godwin Mollel.

Vita ya kisiasa katika Jimbo la Siha, mkoani Kilimanjaro, imechukua sura mpya baada ya Mgombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Godwin Mollel, kudai kuwa mkewe pamoja na msaidizi wake wametekwa na kushambuliwa na watu wasiojulikana.

Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 4, 2025, Dk. Mollel ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya, ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea wakati mkewe akiwa njiani kutoka kumuona mgonjwa, ambapo walivamiwa na kundi la vijana waliokuwa wamezingira gari lao.

"Vijana hao walivamia gari usiku wa kuamkia Agosti 3, wakalivamia na kuvunja vioo. Mke wangu na msaidizi wake walikuwa ndani ya gari hilo," amesema Dk. Mollel kwa hisia.

Mbali na tukio hilo, mgombea huyo pia amedai kwamba kuna gari lilichomwa moto, ingawa hakufafanua gari hilo lilikuwa la nani.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk. Christopher Timbuka, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, amethibitisha kuwa tukio hilo linaripotiwa na tayari liko mikononi mwa Jeshi la Polisi kwa uchunguzi.

“Hatuwezi kusema gari limechomwa moto kwa sasa. Kulingana na taarifa za awali, gari hilo liligonga kingo za calvert na kisha kuachwa pembeni. Baadaye watu walieleza kuwa lilianza kutoa alama lenyewe, na hatimaye wakaona likiungua moto. Lakini tusubiri uchunguzi wa kipolisi utoe taarifa rasmi,” amesema Dk. Timbuka.

Kwa sasa, vyombo vya usalama vinaendelea na uchunguzi kubaini ukweli wa madai hayo ambayo yameongeza mvutano wa kisiasa katika jimbo hilo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.