TRC: Hatuna wakala yeyote wa ukataji tiketi

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 06:45 PM Aug 04 2025
 Ununuzi tiketi mtasndao
Picha: LATRA
Ununuzi tiketi mtasndao

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC), limetoa tahadhari kwa umma, kuhusu tabia inayojitokeza kwa baadhi ya watu kujihusisha na utoaji wa tiketi za huduma ya reli ya kisasa (SGR), kinyume na utaratibu.

Limefafanua kwamba, TRC haina wakala yeyote wa ukataji wa tiketi za SGR na wala haijaingia makubaliano na mtu au taasisi yoyote kutoa huduma hiyo kwa niaba yake.

“Shirika linatoa onyo kwa wale wote wanaojaribu ama kutaka kufanya vitendo vya kughushi tiketi za SGR, kuwa ni kinyume cha Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura Namba 16 na marejeo ya 2002 Kifungu 333 hadi 335, vinavyokataza udanganyifu kupitia nyaraka, mojawapo ni vitendo vya kughushi.”

Limesema, Sheria Namba 10 ya Reli ya Mwaka 2017 Kifungu cha 87, kinasema mtu yoyote atakayejipatia tiketi ya Shirika la Reli, kwa udanganyifu, atakuwa ametenda kosa na adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka miwili au faini isiyopungua shilingi milioni tano na isiyozidi shilingi milioni 10 ama vyote kwa pamoja.

2Kwa mantiki hiyo, Shirika linatoa wito kwa wananchi wote kuhakikisha wanakata tiketi kupitia njia rasmi pekee ambazo ni mtandao au kufika moja kwa moja katika stesheni zetu zote za SGR na kukata tiketi dirishani.

“Kwa taarifa zaidi au msaada, wasiliana nasi bure kupitia kituo cha huduma kwa wateja nambari 0800110042 ama kupitia WhatsApp nambari 0738 594 962  na mitandao  yetu rasmi ya kijamii.”