Hofu matiti kulala yakwaza haki ya mtoto kunyonya

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 04:45 PM Aug 04 2025
Mama akinyonyesha
Picha: Mtandao
Mama akinyonyesha

LICHA ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Wizara ya Afya nchini kusisitiza umuhimu wa unyonyeshaji maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo na kuendelea hadi miaka miwili au zaidi, baadhi ya wanawake, hasa mijini, wanaamua kumwachisha mtoto kunyonya mapema kwa hofu kuwa matiti yao “yatalala” au kupoteza mvuto wa kimwili.

Uchunguzi wa mwandishi umebaini kuwa hofu hiyo, inayochochewa na mitazamo potofu na ukosefu wa elimu sahihi kuhusu afya ya mama na mtoto, inawafanya baadhi ya wanawake kunyonyesha kwa miezi mitatu hadi sita pekee, kinyume cha miongozo ya kiafya. 

Naima Ally (28), mkazi wa Biafra, Kinondoni mkoani Dar es Salaam, anasema alimwachisha mwanawe kunyonya akiwa na miezi minne tu baada ya kushauriwa na marafiki kwamba endapo angeendelea kunyonyesha, matiti yake yangelala. “Nilinyonyesha kwa miezi minne tu, hasa baada ya kurudi kazini. 

Wengine waliniambia nisizidishe miezi sita maana nitaharibu umbo langu,” anasema Naima. Hata hivyo, anasema alijuta baada ya kukumbwa na maumivu ya matiti wakati akimwachisha mtoto, huku akibaini kuwa hata baada ya kuacha kunyonyesha, bado matiti yake yalipoteza umbo kinyume cha matarajio yake.

Baraka Said, mkazi wa Tabata, anasimulia namna mkewe alivyomwachisha mtoto wao kunyonya akiwa na miezi sita, jambo lililosababisha madhara ya kihisia na kiafya kwa mtoto huyo. 

“Mtoto alianza kumpotezea mapenzi mama yake. Hata akiwa mgonjwa, alitaka niwapo mimi. Leo hii ana miaka minne lakini yuko karibu sana na mimi kuliko mama yake,” anasema Baraka. 

Anasema mtoto wao alikumbwa mara kwa mara na maradhi ya mafua, kikohozi na matatizo ya bakteria kwenye damu, hali iliyotafsiriwa na  madaktari kuwa ni matokeo ya kukosa kinga inayopatikana kupitia maziwa ya mama. 

Mwanamke mwingine, Rahma Jamadu wa Ilala Boma, anasema alizingatia ushauri wa madaktari na kumnyonyesha mtoto wake kwa miezi sita mfululizo na hajashuhudia athari zozote katika mwonekano wa maziwa yake. 

Utafiti wa mwaka 2020 uliofanywa na Cianté Pretorius na wenzake kuhusu unyonyeshaji barani Afrika, ulionesha kuwa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwamo Tanzania, zina viwango vya chini vya unyonyeshaji kulinganishwa na nchi nyingine zenye kipato cha chini na cha kati. 

Takwimu za utafiti huo zinaonesha asilimia 55 hadi 75 ya vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano hutokana na mbinu duni za unyonyeshaji, hali inayoweza kuzuilika iwapo kutakuwa na elimu endelevu na utekelezaji sahihi wa miongozo ya kiafya. 

Daktari Bingwa wa Wanawake na Masuala ya Uzazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Lilian Mnabwilu, anasema si kweli kwamba kunyonyesha kwa muda mrefu husababisha matiti kulala, bali ni jambo linalohusiana zaidi na maumbile ya mtu. 

“Wapo waliowanyonyesha miaka miwili na maumbile yao hayajabadi  lika. Pia kuna walionyonyesha kwa muda mfupi au hawakuzaa kabisa, lakini maziwa yao yamepoteza mvuto,” anasema Dk. Lilian. 

Anasema kukosa kunyonyesha kunaweza kumweka mama katika hatari ya kupata matatizo ya kiafya, ikiwa ni pamoja na saratani ya matiti na maambukizi ya usaha kwenye maziwa. 

Kwa mtoto, madhara ni pamoja na kudumaa, kupoteza kinga mwilini, na hatari ya maradhi ya utotoni. “Pia mtoto anayenyonyeshwa hujenga ukaribu wa kihisia na mama yake kupitia harufu, mgusano wa ngozi na joto la mwili,” anasema. 

Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Dk. Donat Shamba, anasisitiza maziwa ya mama ni muhimu mno kwa ukuaji wa ubongo wa mtoto. 

“WHO inasisitiza mtoto aanze kunyonya ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa. Maisha yake ya baadaye, kama kuongea, kutambaa au kuelewa hisia, yanaathiriwa sana na unyonyeshaji wa awali,” anasisitiza Dk. Shamba. 

Msaikolojia Tiba kutoka kituo cha Somedics Polyclinic, Upanga Dar es Salaam, Saldeen Kimangale, anaeleza kuwa mtoto anayenyimwa kunyonyeshwa anaweza kukumbwa na changamoto za kihisia na kisaikolojia katika ukuaji wake. 

“Unyonyeshaji huongeza usalama wa kihisia na upendo wa dhati kati ya mama na mtoto. Kumwachisha mtoto ghafla huondoa ukaribu huo,” anasema. 

Anabainisha pia kuwa baadhi ya wanawake hupata sonona (postpartum depression) baada ya kujifungua, hasa kama hawanyonyeshi, kutokana na kupungua kwa homoni za oxytocin na prolactin, ambazo hutoa utulivu wa akili wakati wa kunyonyesha. 

Wiki ya Unyonyeshaji Duniani huadhimishwa katika zaidi ya nchi 12, ikiwamo Tanzania, kila ifikapo Agosti 1-7.