Dk. Mashinji: Fundisheni maadili kuanzia ngazi za chini kuikomboa jamii

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 06:32 PM Aug 04 2025
Dk. Mashinji: Fundisheni maadili kuanzia ngazi za chini kuikomboa jamii
Picha: Mpigapicha Wetu
Dk. Mashinji: Fundisheni maadili kuanzia ngazi za chini kuikomboa jamii

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Dk. Vicent Mashinji, ametoa wito kwa Ofisi ya Rais – Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhakikisha inaimarisha elimu ya maadili kuanzia ngazi za chini, hususan katika taasisi za elimu, ili kuandaa kizazi cha viongozi waadilifu na jamii yenye maadili bora.

Dk. Mashinji ametoa kauli hiyo alipotembelea banda la Sekretarieti hiyo katika Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

“Tuendelee kuwaelimisha vijana kuhusu maadili. Ni muhimu tukawapa elimu ya kutosha kuhusiana na masuala haya mapema, kwa kuwa elimu ya maadili ndiyo silaha ya kuikomboa jamii ya kesho,” amesema Dk. Mashinji.

Aidha, amesisitiza kuwa jamii inapaswa kurejea kwenye misingi ya utamaduni wa Kitanzania, ikiwemo kurithishana mila na desturi njema ambazo kwa miaka mingi zilisaidia kujenga jamii yenye nidhamu, heshima na mshikamano.

“Nimekuwa nikisema mara kwa mara, tusiporudi kwenye msingi wetu kama jamii, tutaendelea kushuhudia mmomonyoko wa maadili ambao kwa sasa umeenea kwa kasi,” ameongeza.

Awali, Katibu Msaidizi wa Idara ya Ukuaji wa Maadili kutoka Sekretarieti hiyo, Salvatory Kilasara, ameeleza kuwa taasisi hiyo tayari imeanzisha klabu za maadili katika shule za msingi, sekondari na vyuo mbalimbali nchini, ikiwa ni mkakati wa kuwaandaa viongozi na raia wema wa baadaye.

“Dhamira yetu ni kuandaa viongozi waadilifu na wazalendo tangu wakiwa katika hatua za awali za maisha. Hivyo, kupitia klabu hizi, tunawafundisha maadili, uzalendo, uadilifu, na kuwatengeneza kuwa watu wa mfano katika jamii,” amesema Kilasara.