Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari, hususan vya mtandaoni, kuzingatia miongozo na kanuni za uandishi wa habari kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo katika kikao kazi kilichowakutanisha waandishi wa habari kutoka mikoa mbalimbali, Meneja wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, ameeleza kuwa kwa kuwa dunia ya sasa inaendeshwa na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), ni muhimu maudhui ya mtandaoni yazingatie maadili na weledi, hususan katika matangazo ya moja kwa moja (live broadcasts).
"Vyombo vya habari vya mtandaoni vinapaswa kuwa na rasilimali watu muhimu kama mhariri na mhariri mkuu, badala ya kuwa kazi ya mtu mmoja anayefanya kila kitu – kuandika, kuhariri na kupandisha maudhui mtandaoni," amesema Kisaka.
"Hatutavumilia ‘one-man show’ inayokosa uhariri wa kitaalamu."
Aidha, amebainisha kuwa matangazo ya moja kwa moja yanaweza kuwa chanzo cha uchochezi, kwa kuwa huonesha moja kwa moja maeneo ya tukio, muda, na hata mahali walipo askari wa usalama – jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wa taifa.
“Matangazo ya moja kwa moja yanahitaji kuchujwa kwa umakini. Kama kuna machafuko, je ni sahihi kuonesha kila kitu bila kujali athari zake kwa jamii?” amehoji Kisaka.
Akiwaasa waandishi wa habari, Kisaka amesisitiza umuhimu wa kujiepusha na vichwa vya habari vyenye lugha ya uchochezi au vinavyolenga upande mmoja wa kisiasa. Alisema ni wajibu wa waandishi kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi, zisizoegemea upande wowote, na zinazosaidia kudumisha amani.
“Tuache kujenga taswira potofu kuhusu vyama vya siasa vya upinzani. Hawa ni Watanzania kama wengine, wenye mawazo tofauti ya kisiasa. Vyombo vya habari visitumike kuwapaka matope,” amesema.
Pia ametoa wito kwa waandishi kuzingatia uzito wa maneno wanayotumia, hasa katika kipindi hiki nyeti, na kusisitiza kutafuta kauli za kulaani vurugu badala ya kueneza uvumi au taarifa ambazo hazijathibitishwa.
Kwa mujibu wa Kisaka, TCRA inalenga kuona vyombo vya habari vinatumika kujenga, kuelimisha na kuhamasisha ushiriki wa amani katika uchaguzi, badala ya kuwa chanzo cha migogoro.
“Tunataka kuvuka kipindi hiki cha uchaguzi kwa usalama na amani. Vyombo vya habari vina nafasi muhimu sana kuhakikisha hilo linafanikiwa,” amesisitiza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED