Gari la mgombea CCM lachomwa moto usiku, hofu yatawala Igwachanya

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 11:56 AM Aug 04 2025
Gari la mgombea CCM lachomwa  moto usiku, hofu yatawala  Igwachanya
Picha: Mpigapicha Wetu
Gari la mgombea CCM lachomwa moto usiku, hofu yatawala Igwachanya

Gari la Mgombea Udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mawata, ambaye anawania kutetea nafasi hiyo katika Kata ya Igwachanya, Wilaya ya Wanging’ombe, mkoani Njombe, limechomwa moto usiku wa kuamkia Agosti 4, 2025 na watu wanaodaiwa kuwa na silaha za jadi.

Tukio hilo limetokea katika mazingira ya kutatanisha, huku likizua hofu juu ya usalama wa wagombea katika kipindi hiki cha mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho.

Akizungumza na Nipashe Digital kwa njia ya simu leo asubuhi, Mawata alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 10 alfajiri wakati alipokuwa akienda kuchukua gari lake lililokuwa limeegeshwa kwenye gereji jirani.

“Nilikuwa nimetoka nyumbani kwenda gereji kuchukua gari. Nilipofika, nikakuta gari tayari limeungua vibaya na kulikuwa na vijana waliokuwa wameshika mapanga. Miongoni mwao niliyemtambua ni Katibu Mwenezi wa kata,” ameeleza.

Mawata amesema baada ya kuona hali hiyo, alilazimika kuondoka kwa haraka eneo hilo na kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi.

Kwa sasa, jitihada zinaendelea za kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, ACP Mahmoud Banga, ili kupata uthibitisho wa tukio hilo na hatua zinazochukuliwa na Jeshi la Polisi.

Tukio hilo linatokea wakati wa kipindi nyeti cha kura za maoni ndani ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, ambapo kumekuwa na matukio kadhaa ya sintofahamu yanayohusishwa na ushindani wa kisiasa katika baadhi ya maeneo nchini.

Wakati wito ukitolewa kwa vyombo vya dola kuchunguza tukio hilo kwa kina, baadhi ya wachambuzi wa siasa wanahofia kuwa matukio ya aina hiyo yanaweza kudhoofisha misingi ya demokrasia na kuathiri ushiriki wa wananchi katika uchaguzi.