Waziri Chana ahimiza Watanzania kutembelea Maonesho ya Nanenane 2025

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:52 PM Aug 04 2025
Waziri Chana ahimiza Watanzania kutembelea Maonesho ya Nanenane 2025
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Chana ahimiza Watanzania kutembelea Maonesho ya Nanenane 2025

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana amewahimiza Watanzania kutumia fursa ya maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi Nanenane 2025 ili kujifunza mbinu mbalimbali za uzalishaji wa mazao kwa maslahi mapana ya jamii na taifa kwa ujumla.

Waziri Chana amesema hayo leo 4 Agosti, 2025 kwenye viwanja vya  Nanenane  Nzuguni jijini Dodoma ambapo amesisitiza kuwa kutembelea kwenye maonesho hayo itasaidia Watanzania katika kupata elimu ya uzalishaji wa mazao na kujifunza utalii wa vyakula.

“Naomba nitoe rai kwa Watanzania tutembelee maeneo haya ya maonesho kuna bidhaa nzuri, kuna utafiti, kuna elimu, kuna mbegu,  vivutio vya kila aina na pia unapokuja katika maonesho haya unapata elimu unapata elimu ya aina mbalimbali” amesema Waziri Chana.


Aidha, Waziri Chana ameahidi kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo  katika uzalishaji na uongezaji thamani wa mazao ili kuongeza mapato kwa taifa na wananchi na pia kuunga mkono Serikali ya awamu ya sita chini ya  Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inayoendelea kufanya kazi nzuri kwa watanzania.

“Tunapozalisha bidhaa tunaongeza thamani tutapata na mapato lakini tunataka watalii waje kuona utajiri wa Tanzania wa vyakula mbalimbali na ndiyo maana leo tumekuwa na mabanda mahali hapa kuonesha bidhaa zetu za Wizara ya Maliasili na Utalii, tunataka waje kuona utalii wa vyakula, kama ni chai yote hiyo ni aina ya utalii” amesema Waziri Chana.


Katika hatua nyingine Waziri chana amesisitiza kuwa Wizara hiyo itaendelea na mikakati ya kutumia ndege nyuki na  kutenga maeneo ya maalumu  ili kuepukana mwingiliano na migogoro ya mara kwa mara baina ya binadamu na Wanyama wakali na waharibifu kwenye makazi ya binadamu ili kutoa nafasi kwa wananchi kufanya shughuli za kilimo bila bugudha yoyote.

Pia Waziri Chana ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuandaa maonesho hayo katika kanda zote zisizopungua nane hapa nchini hatua inayosaidia wananchi kujifunza mbinu mbalimbali za kilimo, ufugaji na uvuvi.