Niliwanyima fedha polisi wakanipa kesi ya ‘unga'

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 04:37 PM Aug 04 2025
Dawa za kulevya
Picha: DCEA
Dawa za kulevya

MSHTAKIWA Hamisi Mfinanga amedai alikamatwa akituhumiwa kuiba katika ghala, askari polisi wa Buguruni waliomba fedha wamwachie, alipowanyima walimbambika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine.

Amedai hayo katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Godfrey Isaya wakati akijitetea kwa mashtaka yanayomkabili ya kusafirisha dawa za kulevya. 

Akiongozwa na Wakili Habibu Kassim, Mfinanga alidai alikuwa dalali wa vifaa vya ujenzi maeneo ya Buguruni. 

Alikamatwa Buguruni Sheli kwa madai kwamba kuna vifaa vimeibwa. Alidai askari waliomkamata walimwambia awape fedha, ili wasimweke katika hiyo kesi, lakini waliposhindwa kuelewana kwa suala la fedha, walimpeleka Kituo cha Polisi Buguruni kwa ajili ya mahojiano. 

"Nilipofikishwa polisi nikasikia wanasema mimi ni miongoni mwa watu wanaowatafuta kwa upotevu wa vifaa vya ujenzi, nilipelekwa mahabusu," alidai. 

Alidai hakukamatwa Chamazi kama alivyodai shahidi wa nne wa upande wa Jamhuri. Mfinanga alidai alikamatwa Juni 12, 2019 na tangu awekwe mahabusu Polisi Buguruni hakutoka hadi alipofikishwa mahakamani. 

Alidai si kweli kwamba alikamatwa Juni 13 maeneo ya Chang'ombe wilayani Temeke na Kariakoo akisafirisha heroine. 

Mshtakiwa alikana pia kuwa na uhusiano na mshtakiwa mwenzake Ramadhani Mussa na tangu akamatwe hakufikishwa Kituo cha Polisi Tazara kwa ajili ya kushuhudia ufungaji kielelezo. 

Alidai vielelezo aliviona mahakamani, hajawahi kutia saini hati ya ukamataji mali wala kuweka dole gumba katika nyaraka yoyote. 

"Maafisa wa Polisi Kituo cha Buguruni waliniambia ili waniachie niwape hela au la wanitafutie kesi nyingine sababu kesi ni nyingi. "Sijawahi kutenda kosa la kusafirisha dawa za kulevya."

Ninaomba mahakama iniachie, niwe huru," alidai Mfinanga. Akijitetea, mshtakiwa Ramadhani Mussa aliomba mahakama imwachie huru akaangalie familia yake, akikana kuhusika na kosa la kusafirisha dawa za kulevya. 

Alidai anafanya kazi ya kuchomelea vyuma Kariakoo. 

Juni 13, 2019 polisi walifika ofisini kwake, walijitambulisha na kufanya upekuzi. Alidai baada ya upekuzi walipata leseni na namba ya utambulisho wa mlipakodi kisha akawapeleka nyumbani kwake Chang'ombe ambako pia walipekua na kuchukua kadi ya benki, kadi ya umeme na 'memory card'. 

Mshtakiwa alidai shahidi namba tano ambaye ni mjumbe aliyedai alishuhudia upekuzi Kariakoo zikapatikana dawa za kulevya, kwenye upekuzi hakuwapo. 

Alimwona mahakamani akitoa ushahidi. Alidai hamfahamu Mfinanga wala hakuwa na mawasiliano naye yoyote na kwamba hakuwahi kusafirisha kilo 1.082 na gramu 680.03 za heroine.

"Sijashuhudia ufungaji vielelezo, nilikuwa Kituo Kikuu cha Polisi, ninaomba niachiwe huru nikaangalie familia yangu," alidai Ramadhani. 

Akihojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mafuru Moses, Ramadhani alidai mawakili ndio wanatambua kwanini hawakusema kulikuwa na hati nyingine ya ukamataji mali zaidi ya ile ya pakiti ya dawa za kulevya iliyotolewa kama kielelezo mahakamani. 

Akihojiwa Mfinanga alidai hakuwa na leseni kwa sababu ni dalali na alikamatwa kwa tuhuma za wizi na askari wakaomba fedha ili wamwachie. 

Alidai shahidi aliyedai kwamba alimkamata na dawa si aliyemkamata kwa tuhuma za wizi na kwamba hakuwahi kufikishwa Polisi Tazara kwa ajili ya kushuhudia ufungaji kielelezo. 

Akihojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ellen Masululi, alidai aliambiwa vifaa vya ujenzi viliibwa katika ghala Buguruni lakini hakuambiwa ni lipi. 

Baada ya washtakiwa kumaliza kutoa ushahidi, upande wa utetezi ulifunga ushahidi na mahakama ilipanga kutoa hukumu Agosti 19 mwaka huu.

Inadaiwa washtakiwa walikamatwa maeneo ya Chang'ombe, Temeke na Kariakoo Juni 13, 2019 wakidaiwa kusafirisha zaidi ya kilo 1.6 za dawa za kulevya aina ya heroine.