Makatibu wakuu watakiwa kutofanya kazi kwa mazoea

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:36 PM Aug 04 2025
news
Picha Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi, Dk. Moses Kusiluka, akifungua mkutano maalumu wa makatibu wakuu na manaibu kujadiliana utekelezaji wa Dira 2050 na maandalizi ya Mpango wa Maendeleo ya Muda Mrefu.

MAKATIBU Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wote wametakiwa kutofanya kazi kwa mazoea ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hayo ameyasema Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi, Dk. Moses Kusiluka, wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili cha kujadili utekelezaji wa dira hiyo, hatua hiyo inafuatia ikiwa ni siku chache baada ya kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Julai 17 mwaka huu. 

Dk. Kusiluka, akifungua kikao hicho kilichofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha leo, amewataka washiriki kufaham kikamilifu na kuelewa DIRA 2050, pamoja na maudhui ya Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu (LTPP).

Amewasisitiza Makatibu Wakuu kuwa wanapaswa kutoa mchango mpana usioishia katika wizara zao, bali kwa maslahi ya Taifa zima, kwa kuwa huwa wanabadilishana wizara mara kwa mara.

Pia amewataka kuchangia vyema ili kuandaa LTPP inayotekelezeka na halisia, kwa kuwa kupitia LTPP hiyo, Tanzania inatarajiwa kufikia malengo ya DIRA 2050 ikiwemo kuwa na Pato la Taifa (GDP) la dola trilioni moja za Marekani ifikapo mwaka 2050.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk. Tausi Kida alimshukuru Katibu Mkuu Kiongozi kwa kuchukua muda wake kushiriki kikao hicho muhimu kwa utekelezaji wa DIRA 2050 katika kupitia maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu wa miaka 25, Muda wa kati na mfupi ya miaka mitano na mmoja, mtawalia.

Katibu Mtendaji wa NPC, Dk. Fred Msemwa amewakumbusha maagizo yaliyotolewa na Rais, Dkt. Samia wakati wa uzinduzi wa DIRA 2050 tarehe 17 Julai 2025 kuwa yazingatiwe kikamilifu wakati wa utekelezaji.

Dk. Msemwa ametaja maagizo hayo kuwa ni pamoja na mabadiliko ya mtazamo katika utendaji kazi, kila wizara kufanya uhakiki wa sera zilizopo kama zinaendana na DIRA 2050.

Pia kufanyia marekebisho sheria ili ziendane na DIRA 2050, kushirikisha sekta binafsi kama mhimili mkuu, kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini, pamoja na kuendesha kampeni ya uelimishaji wa umma ili kila Mtanzania aelewe maudhui ya dira hiyo.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyewakilishwa na Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole, Wajumbe wa Kikosi Kazi cha kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu (LTPP) wakiongozwa na Balozi, Dk. Asha-Rose Migiro.

Wengine ni baadhi ya wajumbe wa sekretarieti ya baraza la mawaziri, pamoja na watumishi na Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Mipango (NPC).