Kinyozi anaponyolewa na wembe anaoujua kikamilifu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:56 PM Aug 06 2025
Humphrey Polepole
Picha: Mtandao
Humphrey Polepole

KATIKA historia ya utawala na uongozi si lazima uwe na rungu mkononi ili kushiriki udhalimu ukimya mbele ya dhuluma nao ni ushirikiano. Lakini kwa Humphrey Polepole, hata ukimya ulikuwa ni anasa isiyomhusu.

Katika historia ya utawala wa awamu ya tano, jina lake halikuwahi kuwa pembeni. Na hakuwa tu kimya bali alikuwa mchezaji na mchezeshaji. Alikuwa si msemaji tu wa chama tawala, bali mshiriki mahiri wa mfumo uliowaziba midomo waliothubutu kutofautiana. 

Alijenga hoja za kuhalalisha mabavu, akazihubiri kama hekima, na akazilinda kama mwaminifu wa siasa isiyo na utu. Leo, anapojitokeza kwenye majukwaa na mitandao kujenga taswira ya mhanga wa mfumo aliouunda kwa mikono yake na aliouhudumia kwa bidii tunasema kwa ujasiri, kinyozi kanyolewa.

Kwa muda mrefu, Polepole alisimama kama mfasiri wa mfumo, alinyoa fikra, alisafisha hoja na alikemea kila wazo lililokataa kulala upande wa itikadi aliyoipenda. 

Alikuwa sauti ya nidhamu ya kimyakimya na mlinzi wa hofu iliyopewa jina la utulivu. Lakini leo, meza imegeuka, alichokuwa akikishabikia kama desturi na utaratibu, sasa kimegeuka kisu kinachokata mizizi ya nafasi yake na nafsi yake.

 Leo, kinyozi anaonja makali ya wembe aliowatemea wengine na tukumbuke, anayepima vichwa kwa nadharia za wengine, hujikuta siku moja kupimwa kwa kipimo kilekile. 

Siasa haina koo kitakatifu, na mfumo usioweka haki kama msingi huishia kuwameza hata wale walioujenga.

Aliyekuwa sauti ya vitisho vilivyovalishwa tai ya busara, aliyepamba maneno kwa mbwembe huku amevaa joho la unafiki, anaketi kwenye kiti kilekile alichokuwa akikiandaa kwa wengine.

 Anayehubiri leo demokrasia ni yule yule aliyeshiriki kuizika kwa kiburi, ubabe na tabasamu la unafiki, alinyamaza wakati wengine wakipiga kelele kwa maumivu.

Alinyamaza walipotekwa wale waliothubutu kutofautiana nao, aligeuza uso walipozuiwa wapinzani kufanya shughuli zao za kisiasa, haki waliyopewa na katiba, lakini waliyoizuiwa kwa mabavu.

 Hakusema neno lolote yalipojazwa magereza kwa majeruhi wa mfumo alioupamba, hakulia walipoporwa watu mali zao na kunyimwa haki zao mahakamani. 

Alitazama kimya walipopigwa risasi viongozi wa dini na siasa, walipopigwa virungu wanaharakati, walipodhalilishwa wanazuoni, lilipodhibitiwa bunge na walipouawa raia kwa amri za kinyama na kifashisti. 

Badala yake, aliendelea kutoa kauli zenye manukato ya utii kwa mfumo huo huo uliowamwaga damu za watu wasio idadi wala hatia. Mfumo uliozamisha demokrasia kwa risasi, vitisho, na mizengwe ya uchaguzi  mfumo uliogeuza sanduku la kura kuwa jeneza la matumaini.

Na yote haya yalifanyika chini ya utawala wa  awamu ya tano  utawala ambao Polepole aliutumikia kwa ari, akausifia kwa mbwembwe na akaulinda kwa tabasamu la chuki na ufisadi mfumo alioupigia makofi hadharani ‘jahara bil waddii’ au bila shaka, akauita “mfano wa uongozi wa maono.”

Ujasiri wa Kiburi. Nakumbuka kuwa  mwaka 2018, Polepole huyu huyu alikuja Zanzibar, akajigamba mbele ya hadhara kuwa atawafundisha adabu CCM Zanzibar. Ni kauli iliyochochewa na kiburi na batra vilivyompanda kichwani. 

Aliwadharau waliotofautiana naye kwa mtazamo, akaona ubabe kuwa ndio lugha pekee ya kisiasa ili kumfurahisha mtawala, leo, anapotafuta huruma na uhalali wa kisiasa, ni lazima tumkumbushe kuwa alisimama upande wa uovu , ulioamua kutesa badala ya kusikiliza, na kuadhibu badala ya kuheshimu maamuzi ya wananchi. 

Na kwa sababu hiyo, si  mhanga wa mfumo, wala  mwathirika wa mabavu ya dola. Si mpenda demokrasia aliyejeruhiwa. Yeye ni zao la mfumo. Zao la ukimya uliohalalisha dhuluma. 

Leo anapolia kuonewa, ni lazima tumkumbushe kuwa alikuwa sehemu ya kimya kilichotafuna kilio cha wengine.

Kwa taifa linalojifunza, kumbukumbu ni silaha, hatupaswi kuandika upya historia kwa wino wa msamaha unaopuuza ukweli. Polepole ana kila nafasi ya kutubu lakini hapaswi kupewa nafasi ya kujificha nyuma ya kivuli cha uonevu wa kisiasa alioutumikia bila soni, haya wala aibu.

 Sambamba, ukomavu wa kisiasa si kujigeuza mtakatifu baada ya kuhitimisha kazi ya kishetani. Na muhimu zaidi, tusipokumbuka tulikopigwa, tutawapa tena fimbo waliotuchapa. Na kwa hakika  maisha ni duara na  panga la mnyoaji, likikosa nywele  huishia kugusa shingo. Kinyozi kanyolewa na wembe aliowakatia wengine, sasa unamkata kwa ukali ule ule alioukatia wengine.

Balozi wa Tanzania nchini  Cuba na maeneo mengine ya Karibianae, Amerika ya Kati, Colombia, Venezuela na Guyana, alijiuzulu wadhifa huo Julai 13 mwaka huu.

Aliandika barua na kuisambaza  kwenye mitandao yake ya kijamii, akisema kuwa alifikia uamuzi huo baada ya tafakari ya muda mrefu, akisema uamuzi huo si mwepesi, bali umetokana na tafakari ya kina juu ya mwenendo wa uongozi katika nchi yakeu na  uzoefu wake  kama mbunge tangu Novemba 2020.

Alidai hawezi kuendelea kuwa sehemu ya uongozi usiohamasika na utii wa misingi ya katiba ya nchi na chama, haki, maadili, utu na uwajibikaji kwa wananchi, na ameamua kwa hiari yake kujiuzulu nafasi yake na  uongozi na utendaji serikalini.