Serikali kwa kushirikiana na nchi ya Italia kupitia Mradi wa TELMS II, wamekubaliana kuendeleza mageuzi ya Elimu ya Ufundi kwa kuziimarisha Taasisi za elimu ya ufundi ili kuchochea maendeleo nchini.
Katika kikao cha kamati ya pamoja kilichoketi Agosti 5,2025 kikiongozwa na Mwakilishi Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu, Dk. Kenneth Hosea kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, amesema kiasi cha sh. bilioni 54 kitatumika kutekeleza mradi huo.
Amesema mradi huo wa miaka mitano unaoanza 2025/2030 utasaidia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo kwa sababu unalenga kukuza teknolojia, ubunifu na ujasiriamali, pia utaimarisha maendeleo ya nishati endelevu pamoja na suala la uhifadhi mazingira.
Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Sean Coppola, amesema wanajivunia mahusiano mazuri ya kidiplomasia kati yao, hasa kupitia ushirikiano katika miradi ya elimu inayolenga kuwajengea watanzania ujuzi na maarifa.
Mratibu wa Mradi huo, ambaye ni Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Fredrick Salukele amewataja wanufaika wa TELMS II kuwa ni Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST).
Viongozi mbalimbali wa vyuo hivyo walihudhuria kikao hicho wakiwamo Makamu Mkuu wa MUST Prof. Aloys Mvuma, Mkuu wa ATC Prof. Musa Chacha, Mkuu wa DIT Prof. Preksedis Ndomba pamoja na Mkuu wa Taasisi ya ya KIST Dk. Mahmoud Abdulwahab Alawi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED