Wananchi wachangishana fedha kujenga shule iliyotitia

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 01:05 PM Aug 06 2025
Picha za madarasa mapya baada ya kujengwa na wananchi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga
Picha: Shaban Njia
Picha za madarasa mapya baada ya kujengwa na wananchi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga

WANANCHI wa Kata ya Igwamanoni, Halmashauri ya Ushetu, mkoani Shinyanga, wamechangishana fedha zaidi ya Sh. milioni 10 kujenga upya shule ya msingi Igwamanoni iliyotitia.

Shule hiyo baadhi ya madarasa, baada ya mvua kubwa kunyesha Machi, mwaka jana yalititia, huku halmashauri ikiwaunga mkono kwa fedha za mapato ya ndani Sh. milioni 140.

Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1983, ikiwa na vyumba saba vya madarasa na ofisi mbili za walimu, pamoja na matundu ya vyoo 12 na sasa inajumla ya wanafunzi 423 kuanzia darasa la kwanza hadi la saba.

Picha za madarasa mapya baada ya kujengwa na wananchi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mary Lema, ameyabainisha hayo jana, wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa shule ya msingi Igwamanoni kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali Ussi, alipofika kukagua ujenzi na kuweka jiwe la msingi, akiwapongeza wananchi kwa kuungana na serikali kuboresha sekta ya elimu.

Amesema, Machi 12, mwaka jana, majengo ya shule hiyo yalipata nyufa, baada ya mvua kunyesha kwa muda mrefu na kusababisha baadhi ya madarasa kutitia na kuhatarisha usalama wa wanafunzi, hali iliyowafanya wazazi na walezi kuchangisha fedha na kujenga shule mpya katika kijiji cha Iramba.

"Tunawapongeza wazazi na walenzi kwa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto hii na sas ujenzi wake uko katika hatua ya mwisho kukamilika, wanafunzi bado wanaendelea na masomo yao katika vyumba vya madarasa vya sekondari ya Igwamanoni, walipohamishiwa baada ya tatizo hili kutokea," ameongeza Lema.

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Kahama mkoani Shinyanga, ikikagua madarasa yaliyopata nyufa na kusababaisha baadhi kutitia, baada ya mvua kunyesha mwaka 2023
Amesema, halmashauri imewaunga mkono wananchi kwa kutoa kiasi cha Sh. milioni 140 kati yake Sh. milioni 120 ni fedha za mapato ya ndani na Sh. milioni 20 kutoka Mfuko wa Jimbo na mpaka sasa Sh. milioni 129.62 zimeshatumika katika ujenzi huo.

Mmoja wa wakazi wa Igwamanoni, Jumanne Kulwa, amesema walianzisha ujenzi wake kwa awamu 74 za mawe, mchanga 120 pamoja na kokoto awamu mbili, vikiwa na gharama ya zaidi ya Sh. milioni 10 na walifurahishwa zaidi baada ya serikali kuwaunga mkono.

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Kahama mkoani Shinyanga, ikikagua madarasa yaliyopata nyufa na kusababaisha baadhi kutitia, baada ya mvua kunyesha mwaka 2023
Awali akiweka jiwe la msingi, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali Ussi, amempongeza Mkurugenzi Kabojela, kwa hatua alizochukua.

Pia amewapongeza wazazi na walezi, kwa kujitolea kuanzisha ujenzi wa shule upya, kwa kuchangishana fedha na mahitaji mengine. 

“Dhamira ya serikali inalenga kuboresha sekta ya elimu, ili kuhakikish wanafunzi wanasoma katika mazingira bora na kila mwaka bajeti ya wizara sekta hii, imezidi kuimarika zaidi.”