TANZANIA imeshiriki mkutano wa tatu wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu nchi zisizo na mlango wa bahari ambako Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Prof. Godious Kyaharara amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Akifungua Mkutano huo unaofanyika Awaza, Turkmenistan, Rais wa Turkmenstan Serdar Berdimuhamedow amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, kwa nchi za Kusini katika kukabiliana na changamoto za kipekee zinazokumba mataifa yasiyo na bandari.
Pia amethibitisha msimamo wa Turkmenistan wa kutokuegemea upande wowote na kueleleza kuunga mkono utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa 2024 – 2034 wenye lengo la kukuza miunganisho, ustahimilivu na maendeleo endelevu kwa nchi zisizo na bandari.
Katibu Mkuu wa UN, António Guterres, amesisitiza ushirikiano wa kimataifa wenye nguvu na wa vitendo ni muhimu zaidi kwa sasa kuliko wakati mwingine wowote kwa kuwa changamoto za dunia kama za mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kiuchumi, na miundombinu hafifu zinahitaji majibu ya pamoja, hasa kwa nchi zisizo na bandari.
“Diplomasia ya usafirishaji ni kiungo muhimu katika kufungua mustakabali wa biashara kwa nchi zisizo na bandari ili kuendeleza maendeleo jumuishi kwa kuwa maendeleo ya nchi hizo ni mafanikio ya dunia nzima.
“Ustahimilivu wa kijamii na kiuchumi unaweza kufikiwa tu kupitia mikakati inayojumuisha kila mwananchi wa nchi hizo,” amesema.
Mkutano huo umeandaliwa na Umoja wa Mataifa, kwa kushirikiana na Serikali ya Turkmenistan unalenga kutathmini utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Vienna kwa Nchi Zisizo na Mlango wa Bahari wa Mpango kazi wa Vienna wa 2014–2024 na kuweka ajenda mpya ya maendeleo jumuishi kwa kipindi cha miaka kumi ijayo.
Mkutano huo unawakutanisha wakuu wa nchi na serikali, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, sekta binafsi, na wadau wengine kujadili fursa na changamoto zinazozikabili nchi zisizo na bahari ambazo hukabiliwa na gharama kubwa za usafirishaji, utegemezi wa nchi jirani kufikia masoko ya kimataifa, pamoja na changamoto za miundombinu na usafirishaji wa bidhaa.
Malengo mengine ni kukuza ushirikiano wa kimataifa kati ya LLDCs na washirika wa maendeleo, nchi za mpakani, mashirika ya kikanda na sekta binafsi, kuweka msisitizo kwa maendeleo ya kidigitali na teknolojia.
Mkutano huo unaendeshwa chini ya kauli mbiu isemayo “Kufungua fursa kwa nchi zisizo na bahari kwa maendeleo endelevu kupitia ushirikiano wa kikanda na kimataifa”.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED