MJANE mkazi wa Mbezi Makabe, Dar es Salaam, Vedastina Magenda, ameokolewa dakika za mwisho dhidi ya kuuzwa nyumba yake kwa njia ya udanganyifu, baada ya mdogo wake aliyemlea kubadili hati ya nyumba na kukopa Sh. milioni 82.4 kwa jina lake.
Kwa msaada wa kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia, pamoja na ufuatiliaji wa mwandishi wa habari wa Nipashe, mama huyo ameweza kuokoa nyumba hiyo, ambayo ilitarajiwa kuuzwa na kampuni ya udalali ya Majembe Auction Mart Ltd.
Akizungumza kwa uchungu juma lililopita, mama Vedastina alisema kwamba: "Nilimlea huyu mdogo wangu kama mwanangu, nikamsomesha hadi akaoa. Nilipopata shida baada ya kufiwa na mume wangu, nilimwomba msaada wa fedha ili nikarabati nyumba ya kupangisha. Badala yake, alinigeuka, akabadilisha hati ya nyumba kwa jina lake na akaikopea."
Alisema kuwa kwa ujanja, mdogo wake alijitolea “kusaidia” kubadilisha hati kutoka kwa jina la marehemu mume wake, kwa madai kuwa anatoa fadhila. Lakini kumbe alikuwa anatumia ujanja huo kujiwekea jina kwenye hati bila ridhaa yake.
MSHTUKO WA NOTISI
Julai 15, 2025, mama huyo alipokea barua ya notisi ya mnada kutoka kwa Majembe Auction Mart, ikieleza kuwa nyumba hiyo itauzwa ndani ya siku 14 kufidia deni alilokopa mdogo wake kwa kampuni ya CASHME Tanzania.
Barua hiyo ya onyo ilimfikisha katika hali ya kukata tamaa, baada ya kushtuka kwamba hakuwa amewahi kukopa popote na hakuwa na taarifa yoyote ya mchakato huo.
Katika hali ya kukata tamaa, mama huyo alimtafuta mwandishi wa habari wa Nipashe ambaye alimsaidia kumpatia msaada wa kisheria kupitia wanasheria wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
"Mwandishi alinibeba kama dada yake. Akanifikisha kwa wanasheria wa Mama Samia, ambao walinipokea, kunisikiliza na kuchukua hatua haraka sana," alisimulia.
Siku hiyo hiyo, wanasheria hao walimhoji pamoja na upande wa pili, na kisha wakampeleka kwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, aliyeitisha kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
UAMUZI MPYA
Baada ya kikao hicho, Mkuu wa Wilaya alitoa tamko rasmi kuwa: "Nyumba ya huyu mama haitouzwa. Ni mali yake halali, na asisumbuliwe na mtu yeyote. Mama nenda ukaishi kwa amani na watoto wako. Rais Samia amekusaidia."
Kwa machozi ya furaha, mama huyo alisema: "Sikuamini kama kuna watu wanaweza kubeba shida ya mtu kama mimi na kuipigania kwa moyo wa huruma. Nilizoea kudharauliwa kila nilikokwenda, lakini hawa wa msaada wa kisheria walinipa heshima, wakasikiliza, wakachukua hatua."
"Ninashukuru kwa dhati serikali, Kampeni ya Mama Samia, waandishi wa habari na kila aliyesaidia. Nyumba yangu imepona, na sasa ninaishi kwa amani."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED