KUANGUKA kwa baadhi ya vigogo na wanasiasa wakongwe katika mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumeendelea kuzua mjadala mpana, ambapo wachambuzi wa siasa wanasema sababu kuu ni ahadi hewa, uchovu wa sura zilezile na ongezeko la uelewa kwa wapigakura.
Mwanaharakati na mchambuzi wa siasa, Seleman Bishagazi, akizungumza na Nipashe jana, alisema kushindwa kwa baadhi ya wanasiasa waliokuwa wakishikilia majimbo kwa muda mrefu ni matokeo ya kutotekeleza ahadi walizotoa kwa wapigakura wao katika vipindi vilivyopita.
"Sababu ya wakongwe wengi kutemwa katika kura za maoni CCM imesababishwa na ahadi zisizotekelezwa. Watu sasa wanachoka na wanaelewa nani kiongozi mzigo na nani ana uwezo wa kujenga hoja," alisema Bishagazi.
Aliongeza kuwa jamii ya sasa imeelimika zaidi na haitaki tena kurudiwa viongozi walewale waliokosa uwajibikaji. "Watu wanatamani damu changa, wanataka mabadiliko ya kweli," alisisitiza.
Aidha, Bishagazi aligusia suala la rushwa, akisema limeshamiri kwa baadhi ya wagombea ambao alidai walihonga wajumbe ili kushinda kura, jambo ambalo linaharibu taswira ya uchaguzi na kuwanyima nafasi wagombea wenye sifa.
Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shule Kuu ya Elimu, Dk. George Kahangwa, alisema kuanguka kwa vigogo ni ujumbe mzito kutoka kwa wanachama na wapigakura kwamba uongozi si urithi wala mali ya mtu binafsi.
"Ni tathmini ya utendaji. Kama aliwahi kuwa mbunge na akashindwa kwenye kura za maoni, basi kuna mahali alikwama. Inaonesha pia watu hawataki kuona mtu mmoja akiwa madarakani kila mara kana kwamba ni kazi ya kitaaluma," alisema Dk. Kahangwa.
Aliongeza kuwa wakati mwingine kuna michezo michafu ya kisiasa ndani ya vyama, ikiwamo matumizi ya fedha na hongo kwa wajumbe, akisema kuna wagombea wanaoshinda si kwa uwezo, bali kwa kuwa "waliwaona wajumbe sana" na kuwapa kile walichotaka.
"Watu wanakula rushwa, hiyo ndiyo hali halisi. Na kama viongozi wanapatikana kwa njia hiyo, basi ni hatari kwa nchi," alionya.
Dk. Kahangwa aliitaka Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na taasi za kudhibiti rushwa kama TAKUKURU kuongeza nguvu katika kusimamia mchakato wa kura za maoni kama ilivyo katika mitihani ya kitaifa shuleni, ili kuhakikisha viongozi wanapatikana kwa sifa na si fedha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED