Kila watoto 10, mmoja hayupo masomoni, 92% wanajua kusoma na kuandika

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 12:35 PM Aug 06 2025
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdallah Said
Picha: Rahma Suleiman
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdallah Said

KATI ya watoto 10 mtoto mmoja yupo nje ya elimu visiwani Zanzibar na asilimia 92 ya wananchi wa visiwani humo, wanajua kusoma na kuandika.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdallah Said, amesema kuwa sekta ya elimu imepata mafanikio makubwa visiwani, humo hasa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Akizungumza na waandishi wa habari, akiwa ofisini kwake Mazizini, Katibu mkuu huyo amesema miongoni mwa mafanikio hayo katika sekta ya elimu, yametokena na juhudi za serikali katika kuimairsha miundombinu ya elimu ikiwe ujenzi wa shule za kisasa.

Amesema uandikishaji wa wanafunzi kwa ngazi ya elimu ya awali umeongezeka na kufikia asilimia 84.4 kwa mwaka 2024 kutoka asilimia 81.4 na elimu ya msingi umefikia asilimia 103 kutoka asilimia 83.9.

Aidha katika mkuu huyo amesema katika kipindi hicho cha miaka minne ya uongozi huo serikali imefanikiwa kujenga madaras 4,810, shule za gorofa 36 na wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri.

Amesema hatua hizo zimesaidia kuondosha msongamano wa wanafunzi madarasani, wanafunzi kutoingia mikondo miwili shuleni na kupunguza utoro.

Akizungumzia kuhusu TEHAMA, amesema wizara imenunua zaidi ya kompyuta 300 na zingine za mpakato 151 na kuzisambaza shule zote za serikali na wanafunzi wanajifunza kwa elimu masafa.

“Kwa nchi za ukanda wa Afrika, ukitoa nchi ya Afrika Ksini, Zanzibar itakuwa inaongoza kwa vifaa vya TEHAMA katika shule za serikali, hii haijawahi kutokea,” amesema.