Bashungwa aagiza polisi kudhibiti utekaji, ajali na madereva wazembe

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:38 PM Aug 06 2025
Bashungwa aagiza polisi kudhibiti utekaji, ajali na madereva wazembe
Picha: Mpigapicha Wetu
Bashungwa aagiza polisi kudhibiti utekaji, ajali na madereva wazembe

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, ameliagiza Jeshi la Polisi kuendelea kuzingatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha linashughulikia ipasavyo masuala ya jinai, hususan matukio ya utekaji, pamoja na kukomesha ajali zitokanazo na uzembe wa madereva na vyombo duni vya usafiri.

Bashungwa ametoa maagizo hayo leo, Agosti 6, 2025, wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la Kituo cha Polisi Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, lililogharimu zaidi ya shilingi milioni 300.

“Nitumie nafasi hii kulielekeza Jeshi la Polisi kuendelea kuzingatia maelekezo mbalimbali yanayohusu masuala ya jinai, ikiwemo kukomesha matukio ya utekaji, pamoja na kudhibiti madereva wazembe na vyombo vya moto visivyokidhi viwango, ambavyo havistahili kuwa barabarani ili kupunguza ajali,” amesema Bashungwa.

Aidha, Waziri huyo amelitaka Jeshi hilo kuongeza kasi katika upelelezi wa mashauri mbalimbali kwa kushirikiana na vyombo vingine vya haki jinai, sambamba na kuboresha huduma kwa wananchi wanapofika katika vituo vya polisi nchini.

Katika hotuba yake, Bashungwa amesisitiza umuhimu wa Jeshi hilo kudumisha usalama kwa kuhakikisha linakomesha vitendo vya uvunjifu wa amani na uhalifu nchini, ili kulinda tunu ya amani ambayo ni msingi wa maendeleo ya taifa.