Mkurugenzi Mtendaji wa Tamthilia ya Jua Kali,Lamata Leha, ameahidi kuwasomesha bure watoto wawili kila mwaka—msichana na mvulana—kutoka familia zenye hali duni, ili kuhakikisha changamoto za kifamilia haziwazuii kupata elimu.
Leha alitoa ahadi hiyo akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya nne ya wanafunzi wa elimu ya awali na msingi katika Shule ya St. Mark's iliyopo wilayani Mkuranga, mkoa wa Pwani.
“Nikiwa mzazi, ninafahamu changamoto za maisha ambazo mara nyingi huwafanya wazazi kushindwa kuwasomesha watoto wao. Nipo tayari kusaidia watoto wawili kila mwaka kupitia taasisi ya Mutembei,” alisema Leha.
Aliongeza kuwa shule nane zinazomilikiwa na taasisi ya Mutembei ziko katika maeneo mbalimbali nchini, na kwamba iwapo walimu watagundua mtoto anayeshindwa kuhudhuria shule kutokana na ukosefu wa ada, basi yupo tayari kumfadhili kwa gharama zake.
Aidha, alieleza nia yake ya kuwa mlezi rasmi wa shule hizo ili kusaidia kulea na kukuza vipaji vya wanafunzi, akibainisha kuwa aliguswa na vipaji alivyoviona miongoni mwa wanafunzi hao wakati wa mahafali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shule za MHL, Wakili Peter Mutembei, alisema kuwa shule zao hazitoi elimu kwa ajili ya ufaulu pekee, bali pia kuwaandaa watoto kwa maisha kwa ujumla.
"Shule zetu zinazingatia elimu bora, malezi na usalama wa mtoto. Tunashukuru serikali kwa kuweka mazingira wezeshi ya watoto kupata elimu," alisema Wakili Mutembei.
Alieleza kuwa shule zao zinatoa ada nafuu, huku zikiwa na utaratibu wa mikopo kupitia benki mbalimbali kwa ajili ya kusaidia wazazi. Pia hutoa punguzo la ada kwa familia zenye watoto zaidi ya mmoja pamoja na udhamini kwa wanafunzi wanaofanya vizuri kitaaluma au wenye vipaji maalum.
Naye Mkuu wa Shule ya St. Mark's, Devotha January, alisema kuwa kampuni ya MHL inamiliki shule nane nchini, ambapo tano kati ya hizo ni za sekondari na tatu ni shule za msingi.
Alizitaja shule hizo kuwa ni Sekondari ya Ujenzi, St. Matthew's, Victory (zote ziko Mkuranga), St. Mark’s (Kongowe – Mbagala), na Sekondari ya Imagevosa (Iringa). Shule za msingi ni Ujenzi, St. Matthew’s, na St. Mark’s – zote Mkuranga.
Devotha alibainisha kuwa shule hizo zina miundombinu bora inayochangia kutoa elimu bora, na kwamba mwaka huu wanafunzi 30 wanahitimu elimu ya awali, huku 23 wakihitimu elimu ya msingi kutoka St. Mark’s.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED