Moto wawaka vikao uteuzi, upinzani ngumi zarindima

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:19 PM Aug 07 2025
Wagombea wa nafasi ya Urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo (kutoka kushoto), Aaron Kalikamwe na Luhaga Mpina wakifuatilia Mkutano Mkuu wa Chama hicho, jijini Dar es Salaam jana, wenye lengo la kuchagua Mgombea wa Urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa k
Picha: Imani Nathaniel
Wagombea wa nafasi ya Urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo (kutoka kushoto), Aaron Kalikamwe na Luhaga Mpina wakifuatilia Mkutano Mkuu wa Chama hicho, jijini Dar es Salaam jana, wenye lengo la kuchagua Mgombea wa Urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa k

HEKAHEKA za kumpata mgombea urais wa kupeperusha bendera za vyama vya ACT-Wazalendo na Chama cha Wananchi (CUF), Oktoba 29, mwaka huu, zimepamba moto kwa kila chama makada wake kuchukua fomu, huku mikutano ya mchujo ikiendelea.

ACT-Wazalendo kimefanya mkutano wake Dar es Salaam, na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luaga Mpina ambaye alitemwa na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye kura za maoni ni mmoja wa wagombea urais.

Mwingine anayetajwa kuwania nafasi hiyo ni Aaron Kalikawe, majina hayo mawili yalipitishwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho iliyoketi Agosti 5, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, na yamepelekwa kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho ili kupigiwa kura.

Urais wa Zanzibar mgombea ni Othman Masoud Othman ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma wa chama hicho, Shangwe Ayo, ilisema Halmashauri Kuu ilipokea na kuridhia hatua ya mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dorothy Semu kujitoa kugombea nafasi hiyo.

“Kwenye maelezo yake mbele ya Halmashauri Kuu Dorothy ambaye pia ni Kiongozi wa Chama, aliieleza Halmashauri Kuu kuwa alichukua hatua hiyo katika kutekeleza wajibu wake wa kiuongozi.

“Kukiwezesha chama kutekeleza wajibu wake wa kimapambano wa kuiondosha CCM madarakani kwenye Uchaguzi Mkuu, 2025, kwa kuzingatia mazingira ya kisiasa ya sasa nchini,” alisema.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu Ado, alisema Mwenyekiti wa chama hicho, Othman kwamba jina lake pekee litapigiwa kura ili kupitishwa kuwania urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mpina na Kalikawe na Othman maarufu kwa jina la OMO, walitambulishwa kwenye mkutano huo maalum wa uchaguzi uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, ukitanguliwa na Mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho pamoja na Halmashauri Kuu.

Mkutano huo ulichombezwa kwa kaulimbiu ya “Mhuni hakimbiwi’, pia yalitajwa majina ya viongozi wa ngazi zote watakaoteuliwa kushika bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza, alikipongeza chama hicho kwa hatua hiyo ya mchakato wa kushiriki kwenye uchaguzi.

Alisema Msajili kama mlezi wa vyama vya siasa aliwapongeza kwa uamuzi wa kushiriki kwenye uchaguzi kwa sababu ya hiyari, akawataka wawe na siasa za kistaarabu wakikumbuka kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.  

Aliwataka wakumbuke pia kuzingatia kuzuia ukatili wa kijinsia, kudhibiti watu wanaotukana ovyo na kudhalilisha wengine, mazingira ya uchaguzi yawe mazuri ili kila mtu aweze kuwa na amani kushiriki kwenye uchaguzi.

Akizungumza katika mkutano huo kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanafanikisha malengo ya kisiasa, kwamba hakikuchagua kuingia kwenye uchaguzi kwa sababu ya mapenzi bali kinadhamira ya kulinda haki ya kuchagua na kurejesha thamani ya kura ili wananchi wawe na uwezo wa kuamua nani awe kiongozi wao.

Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zito Kabwe, alisema miezi mitatu ijayo inakwenda kutoa tafsiri mpya za siasa za Tanzania kwa mabadiliko.

Wengine walioudhuria mkutano huo ni pamoja na wawakilishi kutoka baadhi ya vyama vya siasa, viongozi wa dini mashirika yasiyo ya kiserikali, wawakilishi wa mabalozi pamoja na mwakilishi wa msajili wa vyama vya siasa nchini.

CUF WATWANGANA NGUMI

Wakati hayo yakijiri, sintofahamu iliibuka jana katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa baadhi ya wajumbe kudaiwa kutwangana ngumi.

Mkutano huo ambao ulifanyika katika Ofisi Kuu za CUF zilizoko Buguruni, Dar es Salaam, umelenga kujadili majina ya wagombea wa nafasi ya urais, ubunge, uwakilishi na madiwani kwa ajili ya uchaguzi mkuu.

Kutokana na sintofahamu iliyojitokeza kwa wajumbe wa mkutano huo, baadhi ya wajumbe walitolewa kwa nguvu katika mkutano huo kwa madai kwamba sio wajumbe halali.

Chanzo cha kuaminika kutoka katika chama hicho kiliiambia Nipashe kuwa wakati vikao vya mkutano vikiendelea, liliingia kundi la watu wanaodaiwa kuwa wameletwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, na kutoa amri kuwa wajumbe ambao sio halali kutoka katika kikao hicho.

“Leo vikao vimeanza, lakini ngumi zimepigwa kwelikweli na baadhi ya wajumbe wameumizwa na baadhi kutolewa nje. Kwa sasa ni wachache tu waliojiteua wanaendelea na vikao,” kilieleza chanzo hicho ambacho ni mmoja wa wanachama wa chama hicho.

Akizungumzia sintofahamu hiyo baada na Nipashe kumtafuta, Mkurugenzi wa Habari wa chama hicho, Mohamed Ngulangwa, alisema kilichofanyika ni mchakato wa kuwatoa watu watano ambao hawakuwa wajumbe katika kikao hicho.

“Ni mchakato uliochukua kama dakika tano tu, kuhakikisha mazingira yanakuwa shwari ili kikao cha Baraza Kuu kiendelee.

“Kwa nafasi wao ni wajumbe ambao wameingia kwenye kikao, lakini waligoma kutia saini orodha ya mahudhurio na utaratibu usipotia saini kwenye kikao chochote hata kama ni cha chama ni jambo la lazima. 

“Waliambiwa wachague kusaini au kutoka nje ya kikao, wakagoma vyote viwili, ndipo nguvu ndogo ikatumika kuwatoa katika mazingira ya kuwapo ukumbini, ilikuwa nguvu salama. Wajumbe waliohudhuria na kutia saini ni 36 kati ya 52,” alisema.

Zanzibar, wanachama watatu wa chama hicho wamejitokeza kuchukua fomu ya kugombea urais wa Zanzibar, akiwamo Hamad Masoud Hamad, Muhamed Habib Mnyaa na Muhamed Mikidadi Khatib.

Wakati chama hicho kikielekea katika uchaguzi mkuu bado kina mgogoro, baadhi ya wanachama wake wamegawanyika makundi mawili, wako wanaomuunga mkono Prof. Lipumba na wengine wasiomuunga mkono.

*IMEANDALIWA na Romana Mallya, Beatrice Moses, Elizabeth Zaya (DAR) na Rahma Suleiman (ZANZIBAR)