Hofu imetanda miongoni mwa wakazi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi, mkoani Mbeya, baada ya kugundulika kuwepo kwa vitu vya ajabu vinavyoaminika kuwa ni vya kishirikina vilivyotelekezwa kwenye makaburi katika eneo la Tanganyika Packers.
Baadhi ya vitu vilivyokutwa makaburini humo ni pamoja na tunguli, nazi zilizopasuliwa, mishumaa, mayai viza, fedha na shanga, hali iliyozua taharuki kwa wakazi wa eneo hilo.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ndola, Joseph Mwakalebela, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikifanyika kwa nyakati tofauti kwenye makaburi matatu ndani ya eneo hilo.
“Vitendo hivi vinatishia amani na vinaathiri kisaikolojia familia za marehemu waliopumzishwa katika makaburi hayo. Tunawaomba wananchi waache kabisa kushiriki au kuhusika na ushirikina,” amesema Mwakalebela.
Ameongeza kuwa uongozi wa kitongoji kwa kushirikiana na vyombo vya dola unafuatilia kwa karibu ili kuwabaini wahusika wa vitendo hivyo na kuchukua hatua stahiki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED