INEC kuwapa wagombea urais magari ya kampeni

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 12:06 PM Aug 28 2025
Gari
Picha: Mtandao
Gari

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza kugawa magari kwa ajili ya wagombea urais wenye kukidhi vigezo vya tume, huku ikitoa uhuru wa kuyanakshi kwa rangi za vyama vyao.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, alisema hayo jana jijini Dodoma wakati akimkabidhi mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, kifaa hicho cha kazi.

Wagombea wengine pia watagawiwa magari hayo kuwarahishia usafiri wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazoanza leo.

Alisema wagombea hao wako huru kuambatana nayo hadi kampeni zitakapokwisha Oktoba 28, mwaka huu.

Gari hilo ni aina ya Toyota Land Cruiser GX-R ambalo mara nyingi huitwa ’Land Cruiser V8’ kwa nchi za Afrika Mashariki, ambapo hutumiwa na viongozi mbalimbali, ikiwamo wabunge.

Magari hayo yanatarajiwa kufanya kazi kwa siku 60 mfululizo kuanzia leo. Mbali na uwezo huo, angalizo la kitaalamu na kwa afya ya injini na usalama, wataalamu wanashauri kulipumzisha gari angalau mara moja, kwa saa 10 hadi 12 za matumizi ya mfululizo.

Pia, thamani yake kwa mujibu wa tovuti kadhaa mtandaoni, inaanzia kati ya Sh. milioni 250 hadi Sh. milioni 300 likiwa jipya.

Ingawa gari ya aina kama hiyo miaka 2016 hadi 2019, iliuzwa kati ya Sh. milioni 90 hadi 150, kulingana na hali ya gari, kilomita zilizotembea na uingizaji wake hadi kufika hapa nchini.

Linatajwa kuwa na uwezo mkubwa barabarani, kwa sababu limeundwa kwa matumizi mchanganyiko wa mjini na barabara ngumu, kwenye mchanga, tope, barafu au mawe bila kuteleza, kupita kwenye mawe, mifereji na barabara mbovu bila kugonga chini. Inaweza kupita kwenye maji yenye kina cha takribani milimita 700.

Kadhalika, yana mfumo wa usalama wa ‘airbags, stability control’ ambao ni mifuko ya hewa unaojifungua ghafla, iwapo gari linapata ajali au mshtuko mkubwa na kusaidia kupunguza nguvu ya mgongano, kumkinga dereva na abiria wasiumie vibaya kichwa, kifua au mikono ama kugonga moja kwa moja ‘dashboard’ au usukani.

Pia, gari aina hiyo inaweza kuwa barabarani kwa muda mrefu, hata saa 24 kwa siku, bila kuzimwa, huku tangi la mafuta likiwa na uwezo wa kuwa na takribani lita 93 hadi 138 kulingana na toleo, na kusafiri kati ya kilomita 600 hadi 1,000 kwa ujazo mmoja uliojaa.