'Kuna upotoshaji uhalali wa Mpina'

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 12:01 PM Aug 28 2025
Luhaga Mpina wa pili kutoka kushoto
Picha: Mpigapicha Wetu
Luhaga Mpina wa pili kutoka kushoto

CHAMA cha ACT Wazalendo kimejitokeza kuondoa sintofahamu kuhusu uhalali wa mgombea wao wa urais, Luhaga Mpina, kikieleza kuwa alijiunga rasmi na chama hicho tangu Julai 29, hivyo alitimiza vigezo vya kikatiba vya kugombea nafasi hiyo ifikapo tarehe ya kuchukua fomu Agosti 4.

Taarifa hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa ACT Wazalendo, Omari Said Shaaban, aliyebainisha kuwa kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, mwanachama mpya anatakiwa kuwa ndani ya chama kwa angalau siku saba kabla ya kupewa ridhaa ya kugombea nafasi ya uongozi.

"Mpina alijiunga tarehe 29 Julai, hivyo kufikia tarehe ya kuchukua fomu alikuwa ametimiza muda unaohitajika. Hakukuwa na ukiukwaji katiba wala sheria yoyote ya chama," alisema Shaaban.

Shaaban alieleza kuwa tayari chama kimefungua kesi mahakamani kupinga uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) wa kuzuia urejeshaji fomu za urais kwa mgombea wao, hatua ambayo anasema imechukuliwa bila haki wala msingi wa kisheria.

"Tume ilimpa Mpina fomu, ikahakiki wadhamini, ikampa barua ya kumtaka arejeshe. Lakini cha kushangaza, baadaye tume hiyo hiyo ikamtaka asirudishe fomu baada ya kupokea barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Hili ni kinyume kabisa cha Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotaka tume kuwa huru," alisema Shaaban.

Alisisitiza ACT Wazalendo haitosimamisha mgombea mwingine wa urais hata kama uamuzi wa tume hautobadilika, kwa sababu wao wanaamini hawajavunja katiba wala sheria yoyote ya uchaguzi.

"Hatua ya tume kutoa uamuzi bila kumsikiliza mgombea, chama chake, au hata kumpa nafasi Msajili wa Vyama kuwasilisha pingamizi rasmi ni jambo la kusikitisha, la ajabu na hatari kwa mustakabali wa demokrasia nchini," alisema.

Wakili huyo pia alizungumzia barua ya malalamiko ya Naibu Katibu wa Uenezi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, MonaLisa Ndala, iliyopinga uhalali wa Mpina kugombea nafasi ya urais kwa madai ya kutotimiza vigezo vya kikatiba.

Shaaban alisema walikuwa wanajiandaa kumjibu Ndala lakini kabla ya majibu hayo kutolewa, tayari alikuwa amekwenda kwa Msajili wa Vyama, jambo ambalo waliliona kuwa ni haki yake, lakini halikuwapa tena fursa ya kujibu rasmi.

ACT Wazalendo sasa inasubiri uamuzi wa mahakama juu ya mgogoro huo, wakiamini kuwa haki itatendeka.

"Kwa mujibu wa katiba yetu na ya nchi, mahakama ndiyo chombo cha mwisho cha utoaji haki. Tunaamini tutapata suluhisho na tutasonga mbele," alisisitiza Shaaban.

AZUIWA INEC

Wakati hali ikiwa hivyo Dar es Salaam, jijini Ddooma jana Mpina alizuiwa kuingia katika ofisi za INEC kurejesha fomu za kugombea, huku tume ikieleza kuwa hakutimiza vigezo vya chama chake.

Mpina aliwasili katika ofisi hizo saa 6:40 mchana akiwa na mgombea mwenza wake, lakini alikutana na zuio kutoka kwa maofisa wa tume waliomwelekeza kuwa hawezi kurudisha fomu hiyo kutokana na kutokidhi masharti ya muda wa uanachama ndani ya chama.

"Tulifika tukiwa tumekamilisha kila kitu kwa mujibu wa katiba na sheria. Kuzuia urejeshaji fomu ni hujuma dhidi ya haki ya kidemokrasia," alisema mmoja wa viongozi wa ACT waliokuwa wameambatana na Mpina nje ya geti la INEC.

SAMIA AREJESHA FOMU

Mgombea urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, jana alikamilisha zoezi la kurejesha fomu yake ya kugombea nafasi hiyo katika ofisi za INEC zilizoko Njedengwa, Dodoma.

Akiambatana na mgombea mwenza wake, Dk. Emmanuel Nchimbi, pamoja na viongozi wakuu wa CCM wakiwamo Katibu Mkuu Dk. Asharose Migiro na Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara Stephen Wasira, Rais Samia aliwasili na kupokewa rasmi na Mkurugenzi wa INEC, Ramadhan Kailima.

Katika zoezi hilo lililochukua takriban dakika 48, Dk. Samia alikabidhiwa rasmi gari la kampeni aina ya Land Cruiser pamoja na dereva, kama ilivyo kwa wagombea wengine walioidhinishwa na tume hiyo.

Mkurugenzi Kailima alisema wagombea hao wametimiza masharti ya Ibara ya 39 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, hivyo wameteuliwa rasmi kuingia katika kinyang’anyiro cha Urais.

Mbali na CCM, wagombea wengine kutoka vyama 16 vya siasa nao wamekamilisha mchakato wa kurejesha fomu na kupokea magari ya kampeni.