Majaliwa awa mbogo taasisi nje ya mfumo

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 01:55 PM Aug 28 2025
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Picha; Mtandao
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameagiza kuchunguzwa kwa viongozi taasisi za umma ambazo bado hazijaunganishwa mfumo wa kisasa wa teknolojia ya Habari na mawasiliano (TEHAMA).

Amesema taasisi hizo zinaweza kuwa na magenge ya uhalifu, hivyo hazitaki taarifa zao ziwe wazi.

Akizungumza jana kwenye Mkutano wa 13 wa Chama cha Wataalam wa Menejmenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) jijini Dar es Salaam, alisema mwisho wa kujiunga na mfumo huo ilikuwa Julai, mwaka huu.

“Mfumo huo unasaidia kuweka uwajibikaji wa haraka, hivyo kila ofisi ya taasisi za umma zinapaswa kujiridhisha kuwa mfumo unafanya kazi sawasawa. Hii inapunguza kazi kwa njia ya makaratasi,” alisema Majaliwa.

Alisema hata taasisi binafsi zinapaswa kuhakikisha zinajiunga kwenye mfumo huo ili kusaidia mawasiliano ya kiutendaji ya haraka.

Majaliwa alisema Kaulimbiu ya mkutano huo ni “Matumizi ya Ofisi Mtandao ni Chachu Kufikia Malengo Makuu Kufikia Dira ya Maendelo ya Mwaka 2050, Shiriki Uchaguzi Mkuu kwa Maendeleo ya Taifa” ina malengo ya kukuza utaalam na weledi wa utunzaji wa nyaraka kuhakikisha zinatuzwa katika hali ya usafi, usiri na usalama.

Aliwataka watumishi hao kudumisha uadilifu na kulinda usiri wa nyaraka za serikali na kuona umuhimu wa kujiendeleza kielimu hasa katika teknolojia ili kumudu mfumo unavyopaswa kuendeshwa pia kuwa wabunifu.

Majaliwa alisema kada hiyo ni wabeba maono wa taasisi, watunza siri za serikali, wasiamizi wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2025-20250 na watunzaji wa kumbukumbu muhimu za kihistoria za taifa kwa ujumla.

Awali Mwenyekiti wa TRAMPA, Devota Mrope, akisoma risala alimweleza Waziri Mkuu Majiliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi kuhusu mfumo huo kwamba  unasaidia kupunguza urasimu.

Pia alisema kuongeza ufanisi katika huduma za serikali, hivyo wanajiona jinsi walivyo na wajibu wa kuhamasisha matumizi yake kwa kuwa ndiyo ndiyo muarobaini wa kuleta maendeleo kwa wakati.

Mrope alisema TRAMPA inatamani Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iwe anakagua na hesabu za masijala.

“Hata wakati Mwenge wa Uhuru unapita uingine pia kukagua ofisi za masijala za manispaa na halmashauri maana ziko mbovu na zinabaki kuwa chakavu kiasi cha kuhatarisha siri za nyaraka zinazotunzwa,zinatoa mwaya kwa adui,” alisema Devota.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora wa Zanzibar, Haroun Ali Suleiman na viongozi wengine kutoka taasisi mbalimbali nchini.