RAIA wa kigeni na baadhi ya waongoza watalii, ambao ni wazawa wa Tanzania, wanahojiwa na mamlaka za serikali wakituhumiwa kuwarekodi maudhui yasiyofaa kuhusu wananchi wanaotoka jamii ya waokota matunda na warina asali wa Kabila la Hadzabe, wanaoishi katika wilaya ya Karatu mkoani Arush.
Jana, Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Lameck Karanga, alisema serikali kupitia mamlaka husika, imeanza kuchukua hatua dhidi ya watu hao.
Kwa mujibu wa Dk. Karanga, ofisi yake kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji, baada ya kuwakamata na kuwahoji raia hao wa kigeni, wamebaini kuwa hawaishi kihalali nchini kutokana na vibali vyao kuisha muda huku akisema hatua stahiki dhidi yao zitachukuliwa.
Aidha, alisema waongoza watalii walioshiriki katika tukio hilo, wamechukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufungiwa kupeleka watalii katika eneo la Wahadzabe.
'Ni kweli jambo hili limetokea na sisi kama serikali tumeanza kuchukua hatua kali. Kwa sababu si jambo jema na si kitendo kizuri kinachofanyika na hawa wenzetu. Kikubwa ni kwamba kimefanyika na watu ambao sio Watanzania.
"Ni watu wa mataifa mengine wanakuja wanachukua picha, halafu wanawanywesha watoto wa Wahadzabe pombe na wakati mwingine wanachukua tena nyama kutoka wanakojua na hata wakati mwingine hatujui zina nini wanawalisha zikiwa mbichi, “ alisema.
" Kwa kweli tutachukua hatua kali sana na hivi leo tunavyoongea tumewakamata tuko nao na tunawahoji. Na hao watu kiukweli wamekuwa wakifanya vitendo hivi vinavyodhalilisha jamii ya Wahadzabe. Kama unavyofahamu ni jamii adimu ambayo inatupa kipato kupitia utalii hapa Karatu," aliongeza.
Mkuu huyo wa wilaya, alisema watu hao wanawafanyia hivyo kwa sababu pengine hali waliyonayo au wakiwa na makusudi yao ya kuiharibia nchi yetu suala la utalii.
"Walikuwa na Watanzania ambao wakati mwingine tunawaita tour guides au ni waongoza watalii na ni wazawa wa Tanzania, ambao nao wanakiuka taratibu.Kwa mfano, hao wenzetu waliofanya haya matukio wameenda bila kibali cha filamu, lakini vilevile wameenda kukaa kule muda mrefu kufanya haya matukio.
"Wako na wenzetu wanaowaongoza kwenye yale maboma ya Wahadzabe. Kwa sababu wao hawajui na wakati mwingine wanatumia hata pikipiki. Kwa hiyo sisi kama serikali tumejikita hadi sasa kuongeza upana wa kuweka vyombo vyetu vya ulinzi katika maeneo hayo ili kuweza kibaini. Tumeenda kuangalia pasport zao (hati za kusafiria) zime-expire (zimeisha muda wake). Wakati mwingine wamekuja hapo kutembea lakini wanajifanya kama watalii," alisema.
Kutokana na tukio hilo, Mkuu huyo wa wilaya alisema Idara ya Uhamiaji imefanya kazi yake vizuri kwa kuwa ilifanya operesheni hiyo na kuwabaini walikuwa wamejificha kwenye nyumba za waendesha utalii. Alisema baada ya uhamiaji kuwakamata, walizuia hati zao za kusafiria ili kuwahoji.
"Kauli ya serikali ni kwamba huu utaratibu haukubaliki wa kwenda kupiga picha kwenye jamii hii ya Wahadzabe bila kuwa na utaratibu. Hatutavumilia, tutachukua hatua kali, "alisema.
Jamii ya Wahadzabe ni moja ya makabila yaliyobaki duniani yanayoendeleza shughuli za uwindaji, ikiishi eneo pekee la kaskazini mwa Tanzania, ikila matunda na mizizi na aina mbalimbali za wanyama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED