Mbuyu wenye taswira ya Bikira Maria wavutia watalii Hifadhi ya Saadani

By Mussa Mwangoka , Nipashe
Published at 03:17 PM Jun 27 2025
Mti aina ya mbuyu ambao upo ndani ya hifadhi ya Taifa ya Saadani ambao una taswira ya Mama Bikira Maria.  Taswira hiyo uonekana vizuri ukiwa umbali wa mita 20.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mti aina ya mbuyu ambao upo ndani ya hifadhi ya Taifa ya Saadani ambao una taswira ya Mama Bikira Maria. Taswira hiyo uonekana vizuri ukiwa umbali wa mita 20.

Mbuyu wenye taswira ya Mama Bikira Maria umekuwa moja ya vivutio vinavyowafanya watalii wengi kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Saadani, iliyopo wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Mwongozaji wa watalii katika hifadhi hiyo, Fredy Neston, amesema mbele ya waandishi wa habari kuwa mbuyu huo umekuwa kivutio kikubwa, hasa kwa wageni wa ndani wenye imani ya dini ya Kikristo, ambao huutembelea kwa ajili ya ibada na sala.

Amesema kuwa mti huo wa mbuyu uligunduliwa mwaka 2019 na mhifadhi mmoja aitwaye Tumaini Magesa, na tangu hapo umekuwa ukivutia waumini wengi, hususan wa madhehebu ya Katoliki, ambao hufika eneo hilo kusali na wengine hurudi kutoa shukrani baada ya kupata kile walichokiomba.

“Tuna vivutio vingi ndani ya hifadhi hii, lakini kwa miaka ya karibuni huu mti wa mbuyu ni kivutio kikubwa. Unavuta watu wengi, na sio wakatoliki tu, bali hata wa madhehebu mengine huja kufanya ibada katika mti huo,” alisisitiza Fredy.

Naye Lazaro Oliver Oliveria, mzee wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kutoka usharika wa Salei mkoani Arusha, alisema kuwa mbali na kuja kupumzika, wamejifunza mambo mengi ya kiimani kupitia mbuyu huo wenye taswira ya dini.

Amesema pia wamepata fursa ya kujifunza historia na mambo ya kale yaliyopo hifadhini, ikiwemo soko la watumwa na mbuyu mwingine ambao wakoloni walikuwa wakiutumia kuwanyonga watumwa waliodhoofika kiafya.

Kwa upande wake, Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Daudi Goroni, alisema kuwa upekee wa hifadhi hiyo unajumuisha mto kukutana na bahari pamoja na kuwa eneo pekee lenye mazalia ya kasa, ambalo halipatikani katika hifadhi nyingine yoyote nchini.