Mkutano maalumu wa wazee wa Shengejuu, Jimbo la Pandani mkoani Kaskazini Pemba, umegeuka kuwa jukwaa la matumaini mapya baada ya Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, kueleza kwa kina dira ya serikali yake kuhusu kuinua uchumi wa wananchi kupitia sekta ya kilimo.
Akihutubia mamia ya wazee na wananchi waliojitokeza, Othman amesema serikali ya ACT Wazalendo imejipanga kuboresha kilimo cha mboga mboga na mazao ya chakula ili kiwe chanzo kikuu cha mapato kwa wananchi wa Pemba, na kuhakikisha wakulima wanafanya shughuli zao wakiwa na uhakika wa kipato, elimu ya kitaalamu na mazingira rafiki ya uzalishaji.
Amesisitiza kuwa serikali itawajengea wakulima taaluma na mafunzo ya kisasa, pamoja na kuwaunganisha na masoko ya ndani na nje ya nchi, hatua itakayowawezesha kujiondoa kwenye utegemezi na umasikini wa muda mrefu.
“Tunataka mkulima wa Pemba awe na thamani, awe na maarifa ya kisasa na apate soko la uhakika. Serikali yetu itakuwa bega kwa bega na wakulima,” amesema Othman.
Aidha, ameahidi kuwa serikali yake itawajengea uwezo maafisa wa kilimo ili wawe chachu ya maendeleo vijijini. Kupitia mpango huo, maafisa hao watakuwa kiungo muhimu kati ya serikali na wakulima, kuhakikisha teknolojia mpya za kilimo zinawafikia wananchi moja kwa moja.
Othman ameongeza kuwa kila baada ya muda fulani, wataalamu wa kilimo Zanzibar watapewa nafasi ya kujiendeleza kielimu, ili kuongeza ufanisi wa sekta hiyo. Baada ya mafunzo hayo, serikali yake itaunda kampuni maalumu ya kilimo itakayoshirikiana nao kwa karibu, ikihudumia wakulima na kuhakikisha kila mmoja anafaidika moja kwa moja na jitihada za kitaifa za maendeleo.
Akigusia suala la mabadiliko ya tabianchi, Othman amesema serikali yake itatekeleza mpango kabambe wa upimaji wa ardhi na maji visiwani Zanzibar ili kubaini maeneo hatarishi na kuchukua hatua za mapema kukabiliana na athari zake.
Ameeleza kuwa wakulima wengi wamekuwa wakipata hasara kutokana na mafuriko na ukame, hivyo serikali itapanga mikakati ya muda mrefu ya kudhibiti athari hizo na kulinda uzalishaji wa kilimo.
Kauli za mgombea huyo zilipokelewa kwa shangwe na matumaini makubwa na wazee wa Shengejuu, ambao wamesema ni mara ya kwanza kwa mwanasiasa kuzungumzia kwa undani maisha halisi ya wakulima wa Pemba.
Mmoja wa wazee waliohudhuria, Mzee Ali Haji, amesema:
“Tumekuwa tukisikia ahadi nyingi, lakini hii ya kuwekeza kwenye kilimo cha kisasa na masoko ni ya kweli na inagusa maisha yetu moja kwa moja.”
Naye Mzee Khamis Hassan ameongeza:
“Sisi wazee tunamuombea kila la kheri. Kama ahadi hizi zitatekelezwa, tutashuhudia kizazi chetu kikiishi maisha bora kuliko tuliyo nayo sasa.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED