Nchimbi aahidi mambo nane Kanda ya Ziwa

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 10:11 AM Sep 08 2025
Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akiwasalimia wakazi wa wilaya ya Ngara mara baada ya kuwasili mkoani Kagera kuendelea na mikutano ya kampeni jana.
Picha:CCM
Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akiwasalimia wakazi wa wilaya ya Ngara mara baada ya kuwasili mkoani Kagera kuendelea na mikutano ya kampeni jana.

WAKATI kampeni za Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani zikishika kasi kwa vyama vya siasa kumwaga sera zao kwa wananchi, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa ahadi nane kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa.

Kampeni hizo zilianza Agosti 28, mwaka huu kwa vyama vya siasa kunadi sera zao, huku CCM kupitia kwa mgombea mwenza wa urais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, akianzia mikoa ya Kanda ya Ziwa kuzisaka kura.
 Akiwa katika mikoa ya Tabora, Geita, Mwanza, Simiyu na Shinyanga, Balozi Dk. Nchimbi aliinadi Ilani ya CCM kwa kutoa ahadi mbalimbali kwa wananchi watakazozitekeleza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo endapo watashinda katika uchaguzi huo.
 
 KIWANDA CHA MADINI
Akiwa mkoani Shinyanga, Balozi Dk. Nchimbi alitoa ahadi ya ujenzi wa kiwanda cha kuchenjua madini mkoani humo, lengo ni kuhakikisha madini yanayochimbwa yanapewa thamani.

 Dk. Nchibi alisema CCM inatambua umuhimu wa madini mkoani Shinyanga na kitakapojengwa kiwanda hicho kitasaidia kuyapa thamani yanayopatikana mkoani humo pamoja na kuongeza mapato ya kigeni.

 Alisema pia CCM itahakikisha mazingira ya uwekezaji yanaboreshwa ili malighafi yaweze kutengenezwa hapa nchini na kukuza pato la taifa.

 WAZAWA KUCHIMBA MADINI
Kadhalika, Balozi Dk. Nchimbi akiwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Masumbwe uliopo Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, aliwaeleza wakazi wa eneo hilo kwamba katika kipindi cha miaka ijayo serikali imedhamiria kuhakikisha madini ya kimkakati yanachimbwa na wazawa au kwa kushirikiana na wageni.

 "Katika kipindi cha miaka mitano ijayo tunakwenda kushughulika na madini ya kimkakati tutahakikisha yanachimbwa na Watanzania wenyewe au kwa kushirikiana na mtu wa nje, lakini Mtanzania awe na hisa ya maana," alisema Balozi Dk. Nchimbi.

 Alisema lengo la kufanya hayo ni kuhakikisha Watanzania wanapata fursa ya uwekezaji katika sekta ya madini pamoja na kasi ya utoaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo itaongezwa.
 
 Vilevile, alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali imetoa leseni za madini 548 wilayani Mbogwe.

 SGR KUKAMILIKA MWAKANI
Akiwa katika eneo la Isaka mkoani Tabora, Balozi Dk. Nchimbi aliwaahidi wakazi wa eneo hilo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha kutoka Dodoma hadi Isaka kilomita 63 zimeshakamilika na sehemu iliyobaki ya kilomita 37 zitakazokamilika mwakani.

 Dk. Nchimbi alisema: "Yaani tunasema mambo ni shwaa...shwaaa. mradi utakamilika. Kwa hiyo niwatoe hofu kila kitu kitakuwa sawa. Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inawajali wanyonge na kuwasikiliza."

 UJENZI WA MIRADI YA MAJI
Balozi Dk. Nchimbi akiwa katika mikao ya Kanda ya Ziwa, alieleza mikakati ya miaka mitano ijayo ya chama hicho ya kumaliza kero ya maji.

 Akiwa mkoani Mwanza Balozi Dk. Nchimbi alisema endapo CCM ikishinda katika Uchaguzi Mkuu itatekeleza miradi ya maji 76 mkoani humo.

 Vilevile, akiwa Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, alisema mojawapo ya mkakati wa kuondoa shida ya maji wilayani Biharamulo CCM itatekeleza miradi 23 ya maji, lengo ni kuhakikisha watu 95 kati ya 100 wapate huduma ya majisafi na salama.

 Akiwa mkoani Geita, Balozi Dk. Nchimbi alitoa ahadi ya kuwekeza nguvu katika ukamilishaji wa mradi wa maji wa miji 13 na kuupanua ili uweze kuhudumia wakazi wengi wa Kanda ya Ziwa.

 Akiwa wilayani Bariadi mkoani Simiyu, Balozi Dk. Nchimbi alisema miaka mitano ijayo CCM ikiendelea kuongoza dola itasimamia ukamilishaji wa mradi wa maji wa Ziwa Victoria ili ufike katika vijiji 23 pamoja na uchimbaji wa visima virefu sita ili kumaliza kero ya upatikanaji wa maji.

 Ahadi nyingine ni kuanzishwa kwa skimu za umwagiliaji katika vijiji 20, mitaro ya umwagiliaji katika vijiji 15 pamoja na kuimarisha eneo la ufugaji kwa kujenga malambo 20.

 NYUMBA ZA BEI NAFUU
Kadhalika, akiwa mkoani Mwanza aliwaahidi wakazi wa mkoa huo kwamba endapo CCM ikishinda uchaguzi huo itaanzisha utaratibu wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu ili kuhakikisha kila mwananchi anamiliki nyumba.

 UJENZI WA MAJOSHO, VIZIMBA, MABWAWA
Akiwa wilayani Rorya mkoani Mara, Balozi Dk. Nchimbi alitoa ahadi ya ujenzi wa majosho 19, vizimba vya kufugia samaki 43 pamoja na ujenzi wa mabwawa yatakayofikia idadi ya zaidi ya 100.

 UBORESHAJI SEKTA YA AFYA
Akiwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa aliahidi uboreshaji wa sekta ya afya katika kipindi cha miaka mitano ikiwamo ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa.

 Akiwa wilayani Mbogwe, aliahidi serikali itaipanua na kuboresha huduma za matibabu katika Hospitali ya Wilaya Mbogwe.

 Pia, itapanua na kuboresha huduma za matibabu katika Hospitali ya Wilaya Mbogwe kwa kununua vifaa vya kisasa, ili wananchi waweze kupata huduma za afya hapo hapo wilayani.