Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, kesho (Jumanne) anatarajia kuanza ziara ya siku mbili mkoani Singida kwa ajili ya kunadi sera na ilani ya chama hicho.
Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Singida, Elphas Lwanji, akizungumza na waandishi wa habari leo (Septemba 8, 2025) amesema Dk.Samia atapokelewa katika Wilaya ya Manyoni na kufanya mkutano wa kampeni kuzungumza na wananchi kwenye viwanja vya soko la kuku.
Amesema mkutano wa pili utafanyika Wilayani Ikungi kwenye viwanja vya stendi na baadaye mchana kutafanyika mkutano mkubwa kwenye viwanja vya Bombadia vilivyopo Manispaa ya Singida.
Lwanji amesema siku ya pili (Jumatano) mgombea urais CCM Dk.Samia ataendelea na ziara ambapo atafanya mkutano kwenye uwanja wa Lulumba wilayani Iramba na hivyo kukamilisha ziara yake mkoani Singida
Lwanji amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea Dk. Samia ambapo atatumia mikutano hiyo kunadi sera na ilani ya chama kwa wananchi na kuelezea mafanikio makubwa ya maendeleo aliyofanya na serikali katika sekta mbalimbali zikiwamo afya, elimu, barabara na kilimo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED