JAMII bado inahitaji elimu kuhusiana na masuala ya ukatili, hususani upande wa watoto na wazazi, ili kutoa taarifa hizo kwa wakati kwenye vyombo vya sheria.
Kambi zilizofanywa kwenye shule tano katika kata za Kwembe na Manzese na shirika la Macho Jamii mwaka 2024, yalifanikisha kuibua kesi 856 za ukatili kutoka kwa wanafunzi.
Kesi hizo ni pamoja kubakwa, kulawitiwa na unyanyasaji wa watoto majumbani mwao, vitu ambavyo waliviainisha watoto wenyewe, huku wakieleza kushindwa kuvitolea taarifa kwa kukosa sehemu sahihi ya kuwasilisha.
Mtoa Huduma wa shirika hilo, Jamila Kisinga, amezungumza na waandishi wa habari, baada ya kukukutana na wanafunzi wa shule ya msingi King'azi, iliyopo kata hiyo, wilaya ya Ubungo.
Amesema matukio ya ukatili bado ni mengi kwa jamii na kwamba yamekuwa yakifichwa na baadhi wanaotendewa kwa kulindana, bila kujua madhara ambayo yanaweza kuwakuta waathirika huku wengine wakikosa watu sahihi wa kuwawasilishia.
Amesema jamii inatakiwa kubadilika na kuwafichua wanaofanya vitendo vya ukatili, ili wachukuliwe hatua na iwe fundisho kwa wengine.
Ameeleza kwamba kati ya kesi 850 zilizoibuliwa mwaka 2024 kati ya hizo 100 zilibainika kuwa ni nzito zaidi na kwamba nane pekee ndio zilifikishwa mahakamani na mbili pekee, zinaendelea kusikilizwa kwenye vyombo vya sheria.
Amesema pamoja na shirika hilo kukosa fedha za ufuatiliaji pia wapo wazazi wanashindwa kufuatilia kesi zao, kutokana na hali zao duni.
Wilson amesema matamanio yao ni kushuhudia wanaofanya vitendo vya ukatili kwa watoto walio na umri chini ya miaka 18 hawapewi dhamana, ili kuondoa taharuki mtaani na pia iwe fundisho kwa wengine.
Pili-Anna Ngome, Mkurugenzi wa Kaya Foundation, amesema wamekuwa wakishirikiana na shirika la hilo, katika shughuli mbalimbali za watoto kuhakikisha ukatili unaondoka kwenye jamii.
Ngome amesema wamekuwa wakiwafundisha wazazi kuhusiana na lishe bora, pia elimu jumuishi kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapelekwa shule.
Kadhalika amesema wamekuwa wakiwatafutia vifaa saidizi watoto wenye ulemavu, huku wazazi wao wakipewa mafunzo ya biashara kupitia vikundi wanavyoviunda kuwaondoa kwenye hali ya utegemezi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED