Dk. Mwinyi: Kampeni za CCM zatoa taswira ya ushindi

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 08:58 PM Sep 08 2025
Dk Mwinyi atetea na Katibu Mkuu CCM
Picha: Mpigapicha Wetu
Dk Mwinyi atetea na Katibu Mkuu CCM

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema mwenendo wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaonyesha taswira ya ushindi na kukubalika kwa chama hicho miongoni mwa Watanzania.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo, Septemba 8, alipokutana na Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dk. Asha-Rose Migiro, aliyefika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo baada ya kuteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo.

Akimpongeza kwa uteuzi huo, Dk. Mwinyi alisema ana imani kubwa na uwezo wa Dk. Migiro katika kuongoza chama hicho, hususan katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu. Pia alieleza kufarijika na mwenendo wa Kampeni za CCM katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara, ambazo zimekuwa zikihudhuriwa na maelfu ya wananchi, hali inayodhihirisha kuendelea kukubalika kwa chama hicho.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dk. Asha-Rose Migiro, alishukuru kwa kuaminiwa na chama hicho kumpa nafasi ya juu ya kiuongozi. Aliahidi kushirikiana kwa karibu na CCM Zanzibar katika utekelezaji wa majukumu ya chama, sambamba na kufanya kazi kwa mshikamano mkubwa wakati wa kampeni.