Singida wasubiri ahadi za Dk. Samia soko alizeti, asali

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:27 PM Sep 08 2025
Dk. Samia Suluhu Hassan.
Picha: Mpigapicha Wetu
Dk. Samia Suluhu Hassan.

Mkoa wa Singida, ulio katikati ya Tanzania, unajulikana kwa mchango wake mkubwa katika kilimo cha alizeti, ambapo hutajwa kama “nyumba ya alizeti.”

Kesho wakulima, wafanyabiashara na wananchi mkoani humo, ni zamu yao kusikia sera na ilani ya CCM kupitia mgombea wake wa urais, Dk. Samia Suluhu Hassan, anayetarajia kutumia siku mbili Singida akifanya mikutano ya kampeni Manyoni, Ikungi na mkutano mkubwa Singida Mjini.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, Mkoa wa Singida una idadi ya watu 2,008,058.

Kabla ya mikutano hiyo, Dk. Samia atakuwa na mikutano asubuhi, wilayani Bahi, mkoani Dodoma, ndipo baadae kubisha hodi Singida, mkoa ambao zaidi ya robo ya mafuta ya kula yanayozalishwa nchini hutokea huko na kuufanya kuwa kitovu cha biashara ya mafuta na mashudu ya alizeti.

Mbali na kilimo, wakazi wengi wanajihusisha na ufugaji wa ng’ombe, mbuzi na kuku wa kienyeji ambao soko lake ni pamoja na Dar es Salaam, hali inayoongeza kipato kupitia nyama, maziwa na ngozi.

Singida pia ni maarufu kwa asali yenye ubora wa hali ya juu, ambayo imepanua wigo wa soko la ndani na kimataifa.

Miundombinu ya reli ya kati na barabara kuu inayounganisha Dodoma na Mwanza imeimarisha zaidi biashara, kwani mkoa huu unatumika kama kitovu cha usafirishaji.

Serikali na wawekezaji binafsi wanazidi kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vidogo vya usindikaji, hivyo kuimarisha ajira na kukuza pato la mkoa.

Singida leo ni mfano wa mkoa unaotegemea rasilimali za kilimo na mifugo kusukuma maendeleo ya uchumi wake.

Maeneo mengine yanayotegeshwa masikio ni pamoja yanayuhusu miundombinu, elimu na sekta ya afya.