‘Kaa mbali na nyoka huyu aina ya swila mwekundu’

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 03:34 PM Sep 08 2025
Nyoka aina ya swila mwekundu
Picha: Mpigapicha Wetu
Nyoka aina ya swila mwekundu

WATAALAMU wa wanyamapori wameonya kuhusu nyoka aina ya ‘Red Spitting Cobra’ (swila mwekundu) wanaotema sumu, na kuripotiwa kusababisha visa vingi vya kung’atwa kwa binadamu na wanyama wa kufugwa.

Wanasema, nyoka huyo anapaswa kuepukwa kwa kila hali kutokana na uwezo wake wa kutema sumu, yenye madhara makubwa kwa macho na ngozi. Hata hivyo, wanaionya jamii kuondokana na dhana kwamba, nyoka hawezi kumng’ata mtoto. 

Kuelekea Siku ya Uhamasishaji wa Kupunguza Ajali za Kuumwa na Nyoka Duniani (World Snakebite Awareness), Septemba 19, kila mwaka, Mkufunzi kutoka Chuo cha Uhifadhi Wanyamapori cha Afrika, Mweka, Tito Lanoy, anasema jamii inapaswa kuwa makini na nyoka wenye hatari zaidi na kuchukua tahadhari, ili wasing’atwe. 

“Nyoka huyu anapohisi tishio, huinua mwili wake, kuonesha shingo yake yenye upana na hutoa mlio wa kutisha kabla ya kutema sumu yake kwa usahihi mkubwa. “Hii ni imani tu, kwenye tafiti zangu zinaonesha watoto nao ni miongoni mwa waliong’atwa na nyoka.” Lanoy alisema ‘Red Spitting Cobra’, iwapo atabanwa au kushikwa, hatasita kung’ata. 

“Ingawa vifo vya binadamu vinavyosababishwa na nyoka huyu si vingi, kung’atwa kunahitaji matibabu ya haraka, sumu inapogusa macho inahitaji kusafishwa mara moja na daktari bingwa. 

“Hupendelea sana vyura na maji, hali inayomfanya kuvamia makazi ya watu hasa usiku akitafuta chakula. Ripoti zinaonesha ndiye kinara wa visa vya kung’atwa kwa binadamu, Kaskazini mwa Tanzania na Kusini mwa Kenya, akifuatiwa na nyoka aina ya Puff Adder,” alisema. 

Alisema sumu ya nyoka huyo ni kali mno, husababisha maumivu makali, kuvimba, kutoka malengelenge na hata uharibifu wa tishu za mwili. “Wataalamu wanasema katika visa vya kung’atwa vibaya, dawa aina ya ‘anti venom’ maalum inapaswa kutumika mara moja. 

“Wanasayansi wanaamini uwezo wa nyoka hawa kutema sumu ulitokana na vitisho kutoka kwa binadamu wa kale, kwani macho yetu yaliyo mbele humfanya apige shabaha kwa urahisi hadi umbali wa futi nane,” alifafanua mtaalamu huyo wa wanyamapori. 

Kadhalika, alisema sumu ya nyoka huyo, inaweza kusababisha muwasho wa macho, kuchoma kornia (cornea) na hata upofu wa muda au wa kudumu, ikiwa haitashughulikiwa haraka. 

“Ingawa sumu yake sio yenye mauti kwa binadamu kama ilivyo kwa nyoka wengine wenye aina hiyo ya sumu, ni hatari sana kwa wanyama wa kufugwa kama mbwa, paka na wanyama wadogo. “Ndani ya mwili wa mnyama, sumu hii huua tishu na kupooza mfumo wa upumuaji wa viumbe wadogo. 

“Kwa rangi, nyoka huyu lazima awe mwekundu. Anaweza kuwa na rangi ya machungwa, manjano, kijivu au kahawia kulingana na eneo analoishi. 

Shingo yake kwa kawaida huwa na alama za giza na chini ya macho kuna mistari ya machozi meusi.” Lanoy alisema nyoka hao pia wanajulikana kwa ulafi hata wa kula wenzao, hali inayowalazimu wadogo kujiepusha na wakubwa ili wasiliwe. 

Alisema nyoka wadogo aina hiyo huwa wanafanya shughuli zao mchana, huku wakubwa zaidi ni usiku. “Nyoka hawa hupatikana Kaskazini mwa Tanzania, Kusini mwa Kenya, Somalia, Djibouti, Ethiopia, Misri, Sudan na Eritrea, wakipendelea maeneo ya savanna kavu karibu na vyanzo vya maji. 

“Ripoti za IUCN zinaonesha hali ya uhai wao bado ni salama na wanapatikana kwa urahisi Afrika Mashariki. “Wataalamu wanashauri iwapo mtu akitemewa sumu machoni au kuumwa, asafishe macho haraka na kutafuta matibabu ya dharura. 

“Wakazi wanashauriwa kutowashika nyoka hawa kwa mikono yao, badala yake wapige simu kwa wataalamu wa kushughulika na nyoka.”