Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdallah, amesema kabla ya ujenzi wa majengo mapya ya kisasa ya Mahakama za Wilaya na Mkoa, vielelezo vya mashauri vilikuwa vikiliwa na panya kutokana na uchakavu na ubovu wa miundombinu ya zamani.
Akizungumza leo, Septemba 8, katika hafla ya ufunguzi wa majengo mapya manne ya Mahakama — moja la Mahakama ya Mkoa na matatu ya Wilaya za Unguja — Jaji Abdallah amesema mazingira duni ya awali pia yalichangia mrundikano mkubwa wa kesi.
Hata hivyo, amebainisha kuwa hali imebadilika baada ya kupatikana kwa majengo mapya, ambapo utendaji kazi umeimarika na upatikanaji wa haki unaharakishwa.
Aidha, amemshukuru Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi kubwa za kuboresha sekta ya mahakama kupitia ujenzi wa majengo mapya katika kila wilaya pamoja na kuongeza idadi ya mahakimu, majaji na makadhi wa kusikiliza mashauri.
“Hatuna deni kwako Mheshimiwa Rais, isipokuwa wajibu wetu sasa ni kuchapa kazi kwa uadilifu na kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa haraka bila kuchelewa,” amesema Jaji Mkuu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED