Nchimbi: Samia ametekeleza miradi 17 aliyoachiwa na Magufuli

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 04:23 PM Oct 16 2025
Mgombea Mwenza wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
Picha: CCM
Mgombea Mwenza wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.

Mgombea Mwenza wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametekeleza miradi 17 aliyoachiwa na mtangulizi wake, Hayati John Magufuli.

Amesema kutoka na uwezo huo Watanzania wanapaswa kumpata tena ridhaa ya uongozi kwa miaka mitano ijayo, ili aendeleze na kukamilisha miradi mingine iliyopo katika Ilani ya CCM ya mwaka 2025-2030.

Amesema hayo leo Oktoba 16 wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma wakati akihutubia wananchi wa wilaya hiyo ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.

"Miradi 17 Rais Samia aliirithi kutoka kwa mtangulizi wake na ameikeleza yote kwa ufasaha. Dunia na Watanzania walikuwa na wasiwasi kama Raid Samia ataweza kuitekeleza. Lakini mchakamchaka alioanza nao nadhani mmeuona. Mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, Reli ya Kisasa na mchakato wa kuhamia makao makuu jijini Dodoma," amesema Dk. Nchimbi.

Dk. Nchimbi amesema hata wakati wa hotuba yake wakati anahapishwa ( Rais Samia) aliihakikishia dunia na Watanzania kuwa ataiendeleza miradi yote iliyoachwa na Hayati Magufuli, jambo ambalo amelifanikisha kwa asilimia 100.

Dk. Nchimbi amesema Rais Samia tangu aingie madarakani Machi 19, 2021ametekeleza miradi ya kimkakati ikiwamo ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma, ukamilishaji wa majengo, taasisi ya serikali mkoani Dodoma, ujenzi wa makazi ya nyumba za watumishi, ukamilishaji wa miradi ya umeme, maji

Dk. Nchimbi amesema: "Dodoma sasa imeanza kufunguka kila mtu anataka kuishi Dodoma. Amesimamia kuongezeka kwa bajeti ya kilimo kutoka.Sh. bilioni 290 hadi Sh. trilioni 1.24. Ameiongeza mauzo ya nyama nje ya nchi kutoka tani 738,000 hadi tani milioni moja".