PDPC, OUT zasaini makubaliano ya kutoa kozi za ulinzi wa taarifa binafsi

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 01:14 PM Nov 14 2025
Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dk. Lameck Mkilia
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dk. Lameck Mkilia

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), imeingia makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa ajili ya kutoa kozi fupi kwa maofisa ulinzi wa taarifa binafsi (DPO),watakaosaidia kutoa elimu kwa wananchi kuimarisha ulinzi na usimamizi wa taarifa binafsi.

Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, imefanyika Novemba 14,2025  jijini Dar es Salaam, ikilenga kuhakikisha taasisi zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi zinatimiza matakwa ya kisheria  ikiwemo  kulinda taarifa na  kujisajili na PDPC.

Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dk. Lameck Mkilia, amesema ulinzi wa taarifa binafsi ni eneo mtambuka linalohitaji   utekelezaji na utoaji wa elimu ili kuhakikisha faragha ya wananchi zinalindwa ipasavyo.

Amesema kupitia makubaliano hayo, OUT na PDPC pia wataandaa maudhui ya pamoja kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda taarifa binafsi na kuandaa mazingira rafiki ya utoaji elimu yanayokidhi mahitaji ya watanzania.

Naibu Makamu Mkuu wa OUT anayeshughulikia Teknolojia za Kujifunzia na Huduma za Mikoa, Prof. Leonard Kweja, amesema kama chuo kilichobobea katika utoaji wa elimu kwa kutumia  TEHAMA kina wajibu mkubwa katika kusimamia masuala ya faragha na ulinzi wa taarifa.

“Makubaliano haya ni hatua muhimu kwa OUT katika kulinda haki binafsi za watu. Katika dunia ya kidigitali, taarifa potofu zina madhara makubwa hivyo ni muhimu kutambua nafasi ya ulinzi wa taarifa katika kulinda jamii na kukuza uchumi,” amesema Prof. Kweja.

Naye Makamu Mkuu wa OUT, Prof. Alex Makulilo, amebainisha kuwa chuo hicho kitaendelea kuzingatia matakwa ya PDPC kwa kuhakikisha taarifa za wanafunzi na za taasisi zinalindwa kwa mujibu wa sheria.

Prof. Makulilo, amesema OUT imeendelea kutekeleza programu zake za elimu  kwa mafanikio kwa sababu ya mtandao wake ulioenea  nchi nzima, ukiwawezesha wananchi wengi kupata elimu bila kulazimika kufika chuoni moja kwa moja.