Bacca, Edmund warejea mazoezini kuivaa AS FAR

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:22 PM Nov 17 2025
news
Picha Mtandao
Bacca, Edmund warejea mazoezini kuivaa AS FAR.

WACHEZAJI wa Yanga ambao walikuwa majeruhi, Ibrahim Hamad 'Bacca' na Edmund John, wamerejea mazoezini kujiandaa na mchezo wa kwanza hatua za makundi, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS FAR ya Morocco, unaotarajiwa kupigwa, Jumamosi ijayo, Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Wachezaji hao wameonekana jana mazoezini kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yanawakabili.

Bacca, hakusafiri na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kwenda nchini Misri kucheza dhidi ya Kuwait kutokana na majeraha.

Hata hivyo, wachezaji wao walianza mazoezi bila kuungana na wengine, badala yake waliwashirikisha waliokuwa majeruhi tu ili kuwalinda wasije kujitonesha na kuendelea kuzidi kuimarika.

Wachezaji hao walifanya mazoezi na Mudathir Yahaya ambaye naye anarejea kutoka kwenye majeraha pamoja na Yao Kouassi, majeruhi wa muda mrefu kwenye kikosi hicho.

"Bacca hatutaki kumwahisha ili asije kujitonesha, lakini kwa sasa yupo kwenye hali nzuri, Edmund unamwona, Mudathir na Yao wao pia wameaanza mazoezi na madaktari wanazidi kuwaangalia kwa karibu kwa hizi siku chache zilizobaki ili tujue kama wanaweza kutumika au la," alisema Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe.

Alisema kikosi cha timu hiyo kinatarajiwa kuondoka kesho kutwa, Jumatano kwa usafiri wa boti kuelekea Zanzibar kwa ajili ya mchezo huo wa Kundi B.

"Tunatangulia Zanzibar kwenda kuwaandalia kipigo 'Waarabu'. Tumewapeleka kule kwa sababu maalum, nadhani baada ya dakika 90 kumalizika kila mmoja atajua sababu ya kuupeleka mchezo Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar," aliongeza kusema Kamwe.

Mbali na timu hiyo, kundi hilo pia lina timu za JS Kablie ya Algeria na Al Ahly ya Misri.

Yanga itaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kushindwa kufuzu hatua ya robo fainali msimu uliopita ilipomaliza nafasi ya tatu ikiwa Kundi A, ambapo timu za Al Hilal ya Sudan na MC Alger ya Algeria zilisonga mbele.