MKURUGENZI wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Rogers Shemwelekwa, ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za wageni au watu wanaotiliwa mashaka kwenye maeneo yao ili uchunguzi ufanyike kwa haraka, huku akibainisha kuwa kuna watu wasiopenda kuona Tanzania ikiendelea kufurahia amani.
Aliyasema hayo jana wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Soko la Mnarani Loliondo aliwasisitiza wafanyabiashara kuendeleza shughuli zao kwa amani na utulivu ili wajipatie kipato halali na kuimarisha uchumi wao.
"Hakuna sababu ya kuwa na hofu katika shughuli zenu kwakuwa ulinzi na usalama umeendelea kuimarishwa na serikali, pia niwatake vijana na wananchi kwa ujumla kulinda amani ambayo ni msingi wa maendeleo ya taifa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Dk. Shemwelekwa akizungumzia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu alisema fedha zipo, hivyo wafanyabiashara wanapaswa kuunda vikundi ili waweze kukopeshwa.
Kadhalika, aliwahakikishia wafanyabiashara hao kuwapa ofisa maendeleo na biashara watakaowasaidia katika usajili wa vikundi ili waweze kunufaika na mikopo.
"Mikopo hii haina riba, jiungeni kwenye vikundi ili mnufaike na fursa hizi za maendeleo," amesema Dk. Shemwelekwa.
Mwenywekiti wa Soko hilo Mohamed Mnembwe aliipongeza serikali kwa ujenzi wa soko jipya ambalo ujenzi wake unaendelea akisema ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara.
Ziara hiyo imetajwa kuwa chachu ya kuimarisha uhusiano kati ya halmashauri na wafanyabiashara, pamoja na kuongeza hamasa ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ndani ya Manispaa ya Kibaha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED