Rais Samia abainisha mageuzi makubwa Sekta ya Madini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:16 PM Nov 14 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan.
Picha: Ikulu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, amesema sekta ya madini imeendelea kuwa kinara katika kuchangia makusanyo ya Serikali, pato la wananchi na uwekezaji kwenye huduma za kijamii kama elimu na afya, hatua iliyochochewa na ongezeko la mchango wake kwenye Pato la Taifa kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020 hadi 10.1 mwaka 2024.

Akizungumza leo Novemba 14, 2025, wakati akihutubia kwenye ufunguzi wa Bunge la 13 jijini Dodoma, Rais Samia ameeleza kwamba mageuzi na mikakati mipya imeiweka Tanzania kwenye mwelekeo thabiti wa kuwa kitovu cha biashara ya madini Afrika Mashariki na Kati ifikapo mwaka 2030.

Mambo Mapya Yaliyotangazwa na Rais Samia

1. Kuanzishwa kwa Mfuko wa Wakfu wa Madini (Mineral Sovereign Wealth Fund)

Rais amesema mfuko huo utawekwa mahsusi kuhifadhi fedha zitokanazo na madini ili kuwapatia manufaa vizazi vijavyo, badala ya kuviachia vizazi hivyo mashimo yasiyo na tija.

2. Madini Kutumika Kama Dhamana ya Mikopo

Serikali itaruhusu mali za madini kutumika kama dhamana ya mikopo ya uwekezaji ili kuongeza mtaji kwa wachimbaji na kuongeza ufanisi katika sekta hiyo.

3. Tanzania Kuwa Kitovu cha Mauzo ya Madini Afrika Mashariki na Kati

Ifikapo mwaka 2030 Tanzania inatarajiwa kuwa eneo kuu la biashara ya madini kutokana na wingi na utofauti wa rasilimali hizo nchini.

Mikakati Endelevu ya Kuimarisha Sekta ya Madini

1. Ujenzi wa Kiwanda Kikubwa cha Kuchenjua Metali (Multi-purpose Refinery)

Kiwanda hicho kitaanza kufanya kazi mwaka 2030 ili kuongeza thamani ya madini hapa nchini, kuzuia usafirishaji wa makinikia nje na kuongeza ajira.

2. Utafiti wa Kina wa Madini Kuongezeka

Serikali itaongeza kiwango cha utafiti kutoka asilimia 16 ya sasa ili kubaini hifadhi halisi ya madini na kuratibu kwa umakini uwekezaji katika maeneo yenye mahitaji makubwa ya kimataifa.

3. Kongani ya Buzwagi Kuajiri Zaidi ya Watu 300,000

Kongani hiyo itajikita katika uzalishaji wa vipuri na bidhaa mbalimbali za madini, hatua inayolenga kujenga nchi inayojiamini kiutengenezaji.

4. Kukamilisha Mkakati wa Taifa wa Madini

Mkakati huo utaainisha aina za madini, maeneo yalipo, kiasi chake na namna ya kuyasimamia ili kuongeza tija ya kiuchumi.

5. Benki Kuu Kuendelea Kununua Dhahabu

BoT itaendelea kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo na wa kati wenye leseni ili kuimarisha akiba ya taifa, kurasimisha biashara na kupunguza utoroshaji.

6. Kukamilishwa kwa Jengo la Tanzanite Exchange Center – Mirerani

Serikali imeahidi kukamilisha jengo hilo ili kuwezesha biashara ya tanzanite kufanyika kwa uwazi, ufanisi na kwa masoko ya kimataifa.

7. Kuimarishwa kwa Masoko ya Madini na Vito

Masoko hayo yataimarishwa ili kuongeza thamani na kupanua wigo wa biashara ndani na nje ya nchi.

8. Leseni Zisizoendelezwa Kufutwa

Serikali itapitia upya leseni zote zinazodumaa na kuzipatia wanaoweza kuzifanyia kazi ili kuongeza uzalishaji.

9. Kuendeleza Wachimbaji Wadogo

Rais Samia amesema Serikali itaendelea kuwapatia wachimbaji wadogo maeneo mapya, mitambo na taarifa sahihi za kijiolojia ili kuwawezesha kuendesha shughuli zao kisasa.