TANZANIA imeibuka mshindi wa jumla kwenye maonesho ya 25 ya wajasiliamali wadogo na wa kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya kampuni ya utengenezaji magari ya KAYPEE Motors kushinda kipengele cha mjasiliamali bora wa mwenye uwezo wa kutunza mazingira.
Imeelezwa kuwa mjasiriamali huyo ahaezalisha magari yanayotumia nishati safi ya umeme ametambuliwa kwenye kundi maalum la wajasiliamali wanaotunza hifadhi ya mazingira.
Tuzo hiyo imetolewa katika maonesho ya wajasiliamali maarufu Jua Kali ambayo yamehitimishwa jana Novemba 16, 2025 Nairobi, Kenya ambapo tarehe hiyo ilikuwa ni siku maalumu ya Tanzania.
Maonesho hayo ya 25 ya wajasiliamali yalihusisha wajasiliamali zaidi ya 3000 toka nchi nane zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akifunga maonesho hayo Waziri wa Viwanda na Biashara wa Kenya, Wycliffe Oparanya, alisema maonesho hayo yalifanyika kwa mafanikio makubwa ikiwa ni miaka 25 tangu yalipoasisiwa mwaka 1999, na kwamba yanasaidia kujenga mshikamano baina ya nchi wanachama.
Waziri huyo alitoa wito kwa nchi wanachama kuongeza bajeti za kusaidia shughuli za wajasiliamali ili wabuni na kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya soko la Afrika Mashari na dunia kote, na kwamba serikali zote zinahimizwa kutafuta suluhu ya kuondoa vikwazo vya kibiashara.
Hata hivyo, alisisitiza kuhusu umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, huku akiwasihi wajasiliamali kutumia mifumo ya kidijitali kukuza biashara zao na kuongeza masoko nje ya mipaka yao.
Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia masuala ya fedha na Biashara, Annette Mutaawe aliwapongeza wanachama wote kwa kujitokeza kwa wingi kwenye maonesho ya mwaka huu ambako alitaja nchi wanachama kuwa ni kutoka Kenya, Uganda, Tanzania, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda, Burundi na Somalia.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Zuhura Yunus aliyeongoza ujumbe wa Tanzania nchini Kenya alisema serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwaratibu na kuwasaidia wajasiliamali ili waongeze tija na ubora wa bidhaa.
Balozi wa Tanzania nchini Kenya Dk. Bernard Kibesse aliwapongeza wajasiriamali Watanzania kwa kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo.
Akizungumzia ushindi huo mjasiriamali kutoka kampuni ya KAYPEE Motors, Mkurugenzi wa Uzalishaji, Rajab Hassan, alisema ushindi waliopata umetokana na uzalishaji wa bidhaa bora kwa miaka 10 mfululizo.
Katika maonesho ya mwaka huu Tanzania iliwakilishwa na wajasiliamali 375 waliotoka Tanzania Bara na Zanzibar ambapo serikali imeratibu wajasiliamali na bidhaa zao kwenda na kurudi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED