Dk Nchimbi: Amani haiwezi kupatikana bila maendeleo jumuishi

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 01:54 PM Nov 17 2025
news
Picha Mpigapicha Wetu
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Emmanuel Nchimbi, katika mkutano wa ICGLR, DRC.

WITO wa amani, usalama na maendeleo kama ilivyosadifu kaulimbiu ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), ulitawala kwenye hotuba za viongozi ikiwemo ya Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliyoisoma kwenye mkutano huo jijini Kinshasa.

Akichangia mjadala juzi katika mkutano huo wenye kaulimbiu ya Kuimarisha Amani na Usalama kwa ajili ya Maendeleo Endelevu kwenye Eneo la Maziwa Makuu, alisema inatambua ukweli wa msingi kwamba maendeleo ya kudumu hayawezi kupatikana bila amani, na amani ya kudumu haiwezi kupatikana bila maendeleo jumuishi na endelevu.

Dk. Nchimbi alieleza kuwa Eneo la Maziwa Makuu limebarikiwa na utajiri mkubwa wa maliasili, zikiwemo madini adimu na rasilimali watu, lakini bado eneo hilo linakabiliwa na migogoro ya kisiasa ya muda mrefu inayochochewa na masuala mbalimbali kama uvunaji haramu wa maliasili. 

“Migogoro hiyo imesababisha majanga ya kibinadamu yakiwemo watu kukimbia makazi yao na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaotokana kwa kiasi kikubwa na uhalifu wa kivita,” alisema.

Aliongeza kuwa sambamba na jitihada mbalimbali za kikanda na kimataifa zinazoendelea hivi sasa kudhibiti migogoro hiyo, Tanzania kama nchi muasisi wa ICGLR imehusika na jitihada mbalimbali za kukomesha migogoro ndani ya kanda ikiwa ni pamoja na kuchangia vikosi vya kulinda amani nchini DRC.

Pia alisema hivi karibuni mwenyeji wa Mkutano wa Pamoja wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliolenga kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa Mashariki mwa DRC.

Aidha, alipongeza jitihada mbalimbali zinazoendelea katika kutafuta ufumbuzi wa migogoro katika nchi za ICGLR.

Jitihada hizo ni pamoja na zile zinazoongozwa na Rais wa Angola, João Lourenço za kutafuta amani nchini DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati; Kusainiwa kwa mkataba wa amani nchini Qatar, kuunganishwa kwa michakato ya Luanda na Nairobi na mkataba wa amani kati ya Rwanda na DRC uliosainiwa chini ya usimamizi wa serikali ya Marekani.

Nchimbi alisema licha ya jitihada hizo, bado kuna changamoto za kiusalama katika nchi mbalimbali, hususan DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Sudan Kusini na Jamhuri ya Sudan. 

Alihitimisha hotuba yake kwa kusisitiza kuwa njia ya kuelekea amani inahitaji ushirikiano na dhamira ya dhati kutoka nchi zote za ICGLR ili kuzikabili changamoto zilizosalia kwa ajili ya kujenga ukanda wenye amani, ustawi na himilivu kiuchumi.