MENEJA Mkuu wa Simba, Dimitar Pantev ameendelea kukisuka kikosi chake kuelekea kwenye mchezo wa makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro de Luanda ya Angola, ambapo kwa sasa amekuwa akiwaelekeza wachezaji wake namna ya kuimaliza timu hiyo kwa mabao mengi iwezekanavyo.
Mchezo huo utapigwa Novemba 23 mwaka huu majira ya saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo, zinasema kuwa kocha huyo amekuwa akiwaonesha wachezaji wake jinsi gani wapinzani wao wanavyocheza, hivyo nao wanatakiwa wafanye nini ili wazuia na kutumia udhaifu wao kupata mabao.
Imeelezwa kuwa mfumo alioutumia juzi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, akiiongoza timu yake kupata ushindi wa mabao 6-0, ndiyo anautengeneza ili utumike kwenye mchezo huo utakaopigwa.
"Kocha amewaonesha wachezaji video za Petro de Luanda jinsi wanavyocheza pamoja na wachezaji wao hatari wa kuchungwa. Pia amewaonesha udhaifu wao, ambao wataitumia kuwaadhibu. Video alizonazo na taarifa ambazo amekusanya kutoka Angola zinaonesha uimara wake uko kwa viungo pamoja na safu ya ulinzi, kwa maana hiyo ametengeneza mfumo wa uchezaji ambao utawavuruga na kuachia mianya,” alisema mtoa habari wetu.
Aliongeza: “Anawaandaa pia viungo wa Simba kuwadhibiti viungo wa Petro de Luanda ili wasifurukute na kuua kabisa mfumo wa uchezaji wa timu.”
Alisema kocha amekuwa akiwasisitiza wachezaji wake hasa wa safu ya ushambuliaji kutofanya makosa wanapokuwa karibu na lango, akiwataka watumie vizuri kila nafasi inayopatikana kwani hahitaji ushindi tu, bali ushindi wa mabao mengi ili kuanza kwa kuongoza kundi.
"Kocha anaamini kuwa kama tukipata ushindi wa mabao mengi, tutaaanza kwa kuongoza kundi na itakuwa ndiyo dira ya kuelekea katika michezo inayofauta," klilisema chanzo hicho.
Petro de Luanda kwa sasa inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Angola ikikusanya pointi 12, ikicheza michezo sita, ikishinda minne na kupoteza miwili.
Timu hiyo imefunga mabao 10 hadi sasa, lakini ikiruhusu matano kwenye nyavu zake.
katika mchezo wake wa mwisho iliyocheza Novemba 9, mwaka huu, ilichapwa bao 1-0 na C D Primeiro de Agosto ambayo pia iliwahi kucheza na Simba kwenye michuano hiyo mwaka 2022.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema maandalizi yanaendelea vizuri kuelekea mchezo huo, akiwataka mashabiki kwenda kwa wingi Uwanja wa Mkapa, ili kuwatisha wapinzani kama ilivyo kawaida.
"Uwanja wa Benjamin Mkapa, ni kama ulijengwa kwa ajili ya Simba, unaweza kuona tumebaki peke yetu hapo, ni wakati wa kuendelea kuwaonesha wageni kuwa siku zote hawatokuwa salama wanapoingia kwenye uwanja huu.
“Ni uwanja unaoogopwa sana na wapinzani wanaocheza na Simba, ile amsha amsha ya mashabiki, kuwahimiza wachezaji wetu na kuwazomea wapinzani, inawachanganya sana kwa sababu pande zote nne zinakuwa za moto kwao," alisema Ahmed.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED