CHAMA cha National League for Democracy (NLD) kimetoa wito kwa vijana wakaopata msamaha wa rais kutokana na vurugu zilizojitokeza wakati wa uchaguzi Oktoba 29, 2025 kutotumia nafasi hiyo kurudia makosa, kikisisitiza umuhimu wa kuzingatia misingi ya amani na utii wa sheria.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Doyo Hassan Doyo, alitoa wito huo wakati akizungumza na gazeti hili jana kutoa maoni yake kuhusu hotuba ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati akizindua Bunge la 13 la Jumhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Hotuba ya rais ilikuwa nzuri na jambo ambalo limeleta faraja na limeoyesha wazi rais ambaye ni mfariji wa Tanzania ni pale ambapo alitoa maelekezo kwa vyombo vya ulinzi kwa vijana wale ambao walifuata mkumbo kwenye vurugu wapewe msamaha,jambo hili ni muhimu kwani kusamehe ni suala la imani na suala la busara,” alisema.
“Mimi niwatake vijana watakaotoka nje kwa msamaha wa rais basi wasijielekeze tena kuleta vurugu katika nchini yao sababu mama ametumia utu katika kuwasamehe vijana wake wa kitanzania na wananchi wake kwamba wengine wanafanya hawaelewi wanafuata mkumbo,”.
Doyo ambaye alikuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, alisema kuwa msamaha uliotolewa na Rais ni ishara ya dhamira njema ya kuendelea kuhimiza maridhiano na mshikamano wa kitaifa, hivyo vijana wanapaswa kuuthamini kwa kutojiingiza tea katika matukio ya uvunjifu wa amani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED