Polisi yashangazwa bodaboda kupiga picha ajali badala ya kuwaokoa walimu

By Gideon Mwakanosya , Nipashe
Published at 10:47 AM Dec 30 2024
Polisi yashangazwa bodaboda kupiga picha ajali badala ya kuwaokoa walimu.
Picha:Mtandao
Polisi yashangazwa bodaboda kupiga picha ajali badala ya kuwaokoa walimu.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limetoa ufafanuzi kuhusu ajali ya gari lililowaka moto na kusababisha vifo vya watu sita, wakiwamo dereva Vicent Milinga na mkewe Judith Nyoni, mwalimu wa Shule ya Msingi Lumalu, wilayani Nyasa.

Hii ni ajali iliyohusisha gari aina ya Toyota Prado lenye namba T 647 CVR ambalo juzi liligonga gema na kupinduka kisha kuwaka moto na kusababisha vifo vya watu sita, wakiwamo walimu wanne wa shule moja. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake mjini Songea, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya alisema ajali hiyo ilitokea saa 1:15 asubuhi katika kijiji cha Buluma, wilayani Mbinga kwenye barabara inayotoka Mbinga kwenda Mbambabay, eneo la kona za Chunya.

Kamanda Chilya alisema kuwa dereva wa gari hilo alifanikiwa kukata kona ya kwanza na alipofika kwenye kona ya pili, gari lilimshinda, likaacha njia na kugonga gema kisha linaingia mtaroni ambako liliwaka moto.

Kamanda Chilya alifafanuwa zaidi kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi uliosababisha dereva kushindwa kulimudu gari, hata likagonga kwenye gema na baadaye kupinduka huku likiwa linaelekea kwenye mtaro.

"Baada ya hapo cheche za moto zilianza kutoka na moto ukawaka na kuwateketeza wote waliomo katika gari hiyo," alisema kamanda huyo.

Hata hivyo, Kamanda Chilya alieleza kuwa kwenye eneo la tukio, wamebaini alikuwapo mwendesha bodaboda ambaye jina lake halijafahamika; mara tu baada ya ajali kutokea, alianza kupiga picha na abiria waliokuwamo katika gari walikuwa wanapiga kelele kwa ishara ya kuomba msaada.

"Huyu mwendesha bodaboda angeweza kuchukua jiwe na kuvunja vioo vya gari hilo ili waweze kutoka, lakini aliendelea kupiga picha ambazo amezisambaza kwenye mitandao," alisema.

Kamanda huyo aliwataja watu wengine waliofariki dunia kutokana na ajali hiyo kuwa ni Damas Nambombe, Dominika Ndau, John Mtuhi ambao wote ni walimu wa Shule ya Msingi Lumalu na Bonifasi Mapunda ambaye ni mfamasia.

Kamanda Chilya alisema mabaki ya miili yao yamechukuliwa na kupelekwa katika hospitali ya serikali wilayani Mbinga ambako ndugu wa marehemu watakabidhiwa baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa vina saba unaohusisha Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Alionya watu wenye tabia ya kupiga picha matukio ya ajali na kuzisambaza kwenye mitandao, akisisitiza wananchi waache tabia ya kujifanya wao ni waandishi wa habari.

"Wawaachie wenye taaluma yao kwani nguvu iliyotumika kupiga picha kwenye tukio hilo ndio ilipaswa itumike kuokoa watu kwenye ajali hiyo," Kamanda Chilya alionya.

Pia aliwataka madereva katika msimu huu wa sikukuu wawe makini kwa kufuata sheria za usalama barabarani ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya ajali.