Ni rasmi Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa mara ya kwanza, kinakuwa na mgombea urais mwanamke, baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kumteua Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwania wadhifa huo.
Hatua hiyo, inaandika historia ndani ya chama hicho tawala, ambacho tangu kuanzishwa kwake 1977 hakikuwahi kuwa na mgombea wa urais mwanamke, ingawa walijitokeza kadhaa na kuishia kwenye michakato ya ndani.
Rekodi ya mbio za urais kwa Rais Dk Samia, zilianzia mwaka 2015 alipokuwa mgombea mwenza wa hayati Dk. John Magufuli na akawa Makamu wa kwanza wa Rais mwanamke hadi Machi 2021.
Baada ya kifo cha hayati Magufuli, Dk. Samia aliapishwa kuwa rais wa awamu ya sita, kwa matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuandika historia ya kuwa mkuu wa nchi wa kwanza mwanamke.
Lakini sasa, Rais Dk. Samia anaingia ulingoni mwenyewe kuzisaka kura za kuukwaa wadhifa huo, jambo lililoibua hisia za wadau wa jinsia, wanaosema hatua hiyo ni mwendelezo wa kiongozi huyo kuvunja mitazamo hasi kuwa, mwanamke hastahili uongozi.
Wadau hao wamekwenda mbali zaidi, wakisisitiza Rais Dk. Samia tayari alishaonyesha uwezo katika kipindi cha miaka minne ya urais wake, hivyo amejaribiwa na ameonyesha uwezo na umahiri katika utekelezaji wa majukumu yake.
Rais Dk. Samia amepitishwa kuwa mgombea wa urais na INEC jana, baada ya kukamilisha taratibu za kisheria ikiwemo kusaka wadhamini katika mikoa yote nchini.
Hatua hiyo, ni baada ya kujaribiwa, kisha uwezo wake ukathibitika na hatmaye CCM ikamuamini kugombea nafasi hiyo, kama inavyoelezwa na mwanasiasa mkongwe, Balozi Gertrude Mongella.
Balozi Mongella amesema kuteuliwa kwa Dk Samia ni uthibitisho kuwa, demokrasia ya Tanzania imevuka mipaka ya hofu dhidi ya wanawake kwenye uongozi, kwa sasa wanaaminiwa.
“Kazi yote niliyoifanya tangu ujana wangu wote nimeumalizia kwenye ajenda kuwa, wanawake wanaweza. Na hili linalofanyika ni uthibitisho wake,” amesema mwanasiasa huyo.
Balozi Mongella ni mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kuwa Katibu Mkuu wa Mkutano wa nne wa Wanawake Duniani (Beijing), uliofanyika nchini China, mwaka 1995.
Kwa mujibu wa mwanaharakati huyo wa haki za wanawake katika uongozi, lazima jamii ikubaliane na ukweli kwamba, inapozungumzwa demokrasia basi iwe inayowahusu watu wote, wanawake na wanaume.
“Tunaposema haki ya kupiga na kupigiwa kura hapa inadhihirishwa kupitia kuteuliwa kwa Dkt Samia kuwa mgombea wa kwanza wa urais kupitia CCM,” amesema.
Balozi Mongella ambaye pia ni mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Bunge la Afrika, amesema hatua hiyo ya Rais Dkt Samia kuwa mgombea urais wa chama hicho, ni sehemu ya matunda ya harakati alizozipambania kuhusu nafasi ya mwanamke katika uongozi.
“Watu wanapomuona Rais Dkt Samia akigombea urais, angalau wanaona matokeo ya kelele nilizokuwa napiga kuhusu haki za wanawake zimeleta matokeo. Huu ni uthibitisho kwamba huyu mama anatokea kwa yule mama aliyekuwa anapiga kelele,” amesema.
Ameeleza hadi CCM inampitisha Dkt Samia, inamaanisha amejaribiwa na kuthibitika kuwa, kiongozi huyo ana uwezo usiotiliwa shaka kwa nafasi anayoiomba.
“Nguvu yake na uwezo wake tunaufahamu, hakuna jambo lisilojulikana, tunamfahamu na chama kinamuamini. Mgombea wa CCM ameaminiwa na chama chake na hasa kwa kutumia utekeleaji wa Ilani ya Uchaguzi. Sio kumwamini kwa maneno, ukisoma utekelezaji wa Ilani, amefanya kazi kubwa,” amesema.
Hoja ya Balozi Mongella, inaendana na Mwanasiasa mkongwe nchini, Anna Abdallah anayesema hatua hiyo inaendelea kuonyesha uthubutu na Dkt Samia anastahili pongezi.
Anna amefafanua kuwa, Dk Samia anastahili pongezi kwa hatua hiyo, kutokana na dhana iliyojengeka katika baadhi ya maeneo kuwa, mwanamke hastahili kuongoza na hivyo anakumbana na vikwazo vingi.
"Hii ya CCM ni funzo kwa vyama vingine. Viongozi wa vyama vyote viendelea kuwahimiza wanawake wagombee. Lazima wagombee," amesema Anna.
Amesema zamani kulikuwa na mwamko mdogo zaidi wa wanawake katika uongozi, kwani wengi waliogopa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, lakini Dkt Samia amevunja miiko na kuwa kielelezo kwa wengine.
Mwanazuoni wa mtaalamu wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benadetha Kilian amesema hatua hiyo inaonyesha Tanzania imepiga hatua katika kuongeza usawa wa kijinsia kwenye nafasi za kisiasa.
Kwa sababu CCM ni chama tawala, Profesa Kilian amesema kumpitisha mgombea wa nafasi kubwa ya kiuongozi kwa ajili ya nchi, ni hatua muhimu na inaandika historia ya nchi kwenye usawa wa kijinsia.
“Duniani kote kuna marais wanawake 24 pekee, Tanzania na yenyewe inaingia kwenye historia hiyo kwanza kwa kuwa na Rais mwanamke lakini zaidi chama tawala kuwa na mgombea urais mwanamke,” amesema Profesa Kilian.
Mwanazuoni huyo, amesema kwa kilichoshuhudiwa ndani ya CCM ni uthibitisho kuwa chama hicho kinaamini mwanamke ni binadamu kama wengine anayemudu uongozi wa kitaifa.
“Juzi CCM ilimteua Dk Asha Rose Migiro kuwa Katibu Mkuu wake, hii ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa CCM, ni hatua nzuri na inaendeleza kuongeza wigo wa wanawake kwenye nafasi za uamuzi,” ameisitiza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED