REA kukamilisha vijiji 151 visivyo na umeme Septemba

By Mary Geofrey , Nipashe
Published at 06:44 PM Jul 15 2024
Mhandisi Mchunguzi wa REA, Jones Oloto.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mhandisi Mchunguzi wa REA, Jones Oloto.

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA), imesema vijiji 151 ambavyo havijafungwa umeme Tanzania Bara, vinatarajiwa kukamilika kabla ya Septemba mwaka huu.

Vijiji vilivyosalia vipo kwa wakandarasi kwaajili ya kukamilishwa ikiwa ni kati ya vijiji 12,318 vilivyopo nchini na kati ya hivyo 12,167 zimeshafungwa umeme.

Mhandisi Mchunguzi wa REA, Jones Oloto, ameyasema hayo juzi mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara(Sabasaba).

Amesema baada ya kukamilisha kufunga vijiji vilivyobaki watabakisha vitongoji 32,427 vinavyotakiwa kufikia na umeme kati ya 64,359 vilivyopo nchini.

Oloto amesema vitongoji 20,000 vitawekewa umeme kwenye mpango wa miaka mitano.

Amesema wataanza na vitongoji 4,000 kila mwaka kwa kuanzia mwaka mpya wa fedha 2024/25 kumaliza katika kipindi cha miaka hiyo mitano ambapo vitabaki vitongoji zaidi ya 8,000 ambavyo vitamalizwa kwa kipindi cha miaka mingine miwili na nusu.

“Baada ya kumaliza tutahamia hatua ya nyumba kwa nyumba. Kule vijijini kuna nyumba nyingine zinakuwa mbali na miundombinu lakini kuna nyumba mpya zinaibuka zinatakiwa kufungwa umeme pamoja na taasisi za afya ambazo zinajengwa,” amesema.

1

Ameongeza kuwa, kuna miradi maalum ya kupita kwenye taasisi za afya, elimu, migodi, vituo vya polisi na mahakama ndogo ambao idadi yake ipo na wataendelea kutoa huduma.

“Kila sekta tunayogusa ni lengo la kuinua wananchi kiuchumi kwasababu umeme unarahihisha shughuli za wananchi kiuchumi,” amesema.

Aidha, amesema katika kusambaza nishati safi ya kupikia vijijini mwaka ujao wa fedha watagawa mitungi 600,405 kwa maana ya ruzuku kwa wananchi wa vijijini kwa punguzo la asilimia 50.

Amesema waliopo eneo la pembezoni mwa miji watalipa kwa punguzo la asilimia 20 kwaajili ya nishati ya kupikia.

Oloto amesema pia tayari walishajenga mifumo ya bayogesi kwenye majiko ya nyumbani 725 kwa Tanzania bara na mifumo ya taasisi 52 kwenye shule za sekondari na kambi za jeshi.

“Huu ni mwendelezo wa kazi kubwa ambayo tumeshafanya huko nyuma, kutokana na uzinduzi wa nishati safi ya kupikia na maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.

2